Dunia inavyomkumbuka, Dk. Ronald Ross mgunduzi wa mbu, Malaria

August 20, 2025 6:48 pm · Sauda Ndaza
Share
Tweet
Copy Link

  • Ugunduzi huo uliweka msingi wa tafiti za baadaye za kinga na tiba ya Malaria.

Dar es Salaam. Kila ifikapo Agosti 20, dunia huadhimisha Siku ya Mbu Duniani ikiwa ni kumbukumbu ya ugunduzi mkubwa uliofanywa na Dk. Ronald Ross, daktari na mtafiti wa tiba kutoka Uingereza aliyebadilisha historia ya mapambano dhidi ya Malaria. 

Mwaka 1897, Ross aligundua vimelea vya Malaria ndani ya tumbo la mbu jike aina ya Anopheles, na kwa mara ya kwanza kuthibitisha kwamba mbu ndiye msambazaji mkuu wa ugonjwa huo.

Ugunduzi huo uliweka msingi wa tafiti za baadaye za kinga na tiba ya Malaria, huku Ross akiendelea kufanya utafiti wa kina hadi kuthibitisha mzunguko wa maisha ya vimelea hivyo.

Ever Present, Ever Relevant: Donald Ross at 150

Dk, Ronald Ross aliyegundua vimelea vya Malaria ndani ya tumbo la mbu jike aina ya Anopheles, na kwa mara ya kwanza kuthibitisha kwamba mbu ndiye msambazaji mkuu wa ugonjwa huo./Picha google.

Kwa mchango huo mkubwa, alitunukiwa Tuzo ya Nobel ya Fiziolojia mwaka 1902, na kuwa mwanasayansi wa kwanza wa Uingereza kupata heshima hiyo.

Leo hii kumbukumbu ya ugunduzi wake huenziwa kama sehemu ya juhudi za kuelimisha jamii kuhusu mbu na madhara wanayosababisha.

Lakini mbali na malaria, Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa mbu ni “wanyama wauaji zaidi” duniani.

WHO inakadiria kuwa magonjwa yanayosababishwa na mbu kama malaria, dengue, chikungunya na Zika husababisha vifo zaidi ya 700,000 kila mwaka, sawa na asilimia 17 ya magonjwa yote ya kuambukiza duniani.

Nchini Tanzania watu 1,503 walipoteza maisha kutokana na Malaria ambapo mikoa ya Tabora, Mtwara,Kagera ,Shinyanga na Mara ikitajwa kuwa vinara wa maambukizi ya ugonjwa huo.

Magonjwa makuu yanayosambazwa na mbu yameendelea kuwa tishio duniani ikiwemo Homa ya dengue, inayosambazwa na mbu wa Aedes aegypti, Malaria inayoenezwa na Anopheles pamoja na  chikungunya.

Mosquitos - Federation Council

Magonjwa makuu yanayosambazwa na mbu yameendelea kuwa tishio duniani ikiwemo Homa ya dengue, inayosambazwa na mbu wa Aedes aegypti/Picha google.

Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa watoto wadogo, wazee, wanawake wajawazito na watu wenye kinga dhaifu wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata madhara makubwa ya magonjwa yanayosambazwa na mbu.

Ili kupunguza maambukizi, wataalamu wa afya wanashauri jamii kuondoa mazalia ya mbu kwa kumwaga maji yaliyotuama, kutumia vyandarua vyenye dawa, kufunga madirisha na milango kwa wavu, pamoja na kushirikiana kwenye kampeni za usafi.

Tangu ugunduzi wa Ronald Ross, mapambano dhidi ya malaria na magonjwa mengine yanayosababishwa na mbu yameendelea kuwa ajenda ya kimataifa. 

Siku ya Mbu Duniani si tu kumbukumbu ya kihistoria, bali pia ni wito kwa dunia kuendelea kuwekeza katika utafiti, kinga na tiba ili kuokoa mamilioni ya maisha kila mwaka.

Imeandikwa na Swaumu Nyunguru pamoja na Sauda Ndaza

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks