AI jinamizi lingine elimu ya juu Tanzania?
- Baadhi ya wahadhiri, wanafunzi na wengineo wanahofu AI inaweza kudidimiza elimu ya juu nchini.
- Wengine wanaona ni fursa itakayoongeza ufanisi wa kujifunza.

Dar es Salaam. Baadhi ya wanafunzi wanaosomea upasuaji katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) walikuwa wakionyesha tabia iliyomshangaza sana mkufunzi wa somo hilo kwa muda mrefu.
Wanafunzi hao walikuwa wakiandika ripoti bora za utafiti wanaoufanya kiasi cha kumvutia kila mtu.
Hata hivyo, inapofika hatua ya kuwasilisha (presentations) ripoti hizo wengi hushindwa kabisa kudadavua walichokiandika kana kwamba hakikuandikwa na wao.
Mwenendo huo ulimtia shaka mhadhiri wao, Dk. Abdurahman Amin wa MUHAS kutokana na mabadiliko makubwa ya wanafunzi hao ndani ya muda mfupi.
Ili kubaini ukweli, ilimchukua muda kidogo Daktari huyo bingwa wa upasuaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kugundua kuwa wanafunzi wake hutumia akili unde ama mnemba (AI) kuandika ripoti zao.
“Kusipokuwa na udhibiti wa maana, tutazalisha kizazi ambacho hakijitumi na ambacho si bunifu kabisa,” anasema Dk. Amin akionyesha kukatishwa tamaa na matumizi yasiyo na maadili ya AI kwa wanafunzi wake.

Wanafunzi wa udaktari licha ya kwamba wanahimizwa kutumia teknolojia kujifunza wanahitajika kuzitumia kwa weledi na maadili kwa kuwa kazi wanayosomea inashikilia uhai wa watu.
Matumizi ya AI kwa wanafunzi wa vyuo vikuu hayapo kwa wanafunzi wa Dk. Amin pekee. Tanzania kama mataifa mengine duniani, inashuhudia mageuzi makubwa katika mfumo wa elimu ya juu ambapo wanafunzi wa vyuo vikuu wanatumia AI si tu kama nyenzo ya kujifunza, bali kama msaidizi wa kila siku katika kazi zao za kitaaluma.
Sehemu kubwa ya wanafunzi waliohojiwa na Nukta Habari wanakiri kutumia AI kwenye masomo huku baadhi wakitumia kwa hofu kuwa itaua fikra zao za kufikiri na kuvumbua mambo mapya.

Musa George mwanafunzi wa Shahada ya Uandishi wa Habari wa Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya UDSM anasema anaitumia vyema AI na ni mkombozi wake mpya katika taaluma yake ya Uandishi wa Habari.
George anasema kuwa amekuwa akitumia AI kufanya kazi zake ikiwemo kuandika ripoti mbalimbali, kutafuta mawazo mapya na hata kufanya ‘assignment’ kwa urahisi na haraka kuliko hata kupitia maktaba na nukuu kutoka kwa walimu.
Ngumu kurudi nyuma
Baadhi ya wanafunzi wanasema kwa hali ya sasa vyuo vikuu havina namna zaidi ya kutafuta njia rafiki itakayohimiza matumizi sahihi ya AI.
Mwanafunzi wa Shahada ya Mahusiano ya Umma wa SJMC Lucy Mtana anasema ni vema vyuo vikaweka sera na miongozo katika matumizi ya kitaaluma.

“AI ndipo dunia inapoenda,” anasema Mtana huku akibainisha kuwa wanafunzi hawawezi kuacha kutumia na njia pekee ya kuepuka athari hasi ni kwenda nayo kwa mipango madhubuti.
Kima cha matumizi ya AI kinatofautiana kidogo baina ya wanafunzi kutokana na kozi wanazosoma. Licha ya wanafunzi wa udaktari na uhandisi kutumia AI kujifunzia na kufanya mazoezi wengi bado wana mashaka nayo.
‘Inaua fikra taratibu’
Rita Subira, mwanafunzi wa mwaka wa nne wa Shahada ya Udaktari wa Kinywa na Meno, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) anasema licha ya AI kurahisisha kazi anahofia inaweza kuwa ni sumu “tamu” inayoua fikra kwa upole.
Subira, ambaye hutumia AI katika kazi zake za kitaaluma, anaeleza kuwa wanafunzi wengi hutumia AI kufaulu na kurahisisha kazi kwa haraka ili wasipitilize muda waliowekewa kuwasilisha kazi wanapopewa na wakufunzi wao.

Tabia hiyo, anaeleza kuwa inaweza kuwalemaza wanafunzi na kuzalisha wataalamu wasio na weledi hapo baadae, kitu ambacho amekitaja kama hatari inayoweza kuleta madhara makubwa hasa kwa taaluma nyeti kama udaktari.
“Atakapokutana na kesi mpya kwa mgonjwa, hawezi kufanya maamuzi ya haraka mpaka airudie tena AI,” anasema Subira akionyesha mashaka yake akihusianisha na maadili ya taaluma hiyo.
Mamia wanatumia AI vyuoni
Wanafunzi hao si pekee wanaotumia AI katika masomo yao nchini. Utafiti uliochapishwa hivi karibuni na Jarida la Habari za Teknolojia la East African Journal of Technology ukihusisha watafiti kutoka Chuo cha Uhasibu (TIA) kilichopo jijini Mbeya unaonyesha kuwa takriban nusu ama asilimia 47.5 ya wanafunzi hutumia AI kuandika kazi zao.
Kwa mujibu wa utafiti huo, wanafunzi wanne kati ya 10 au asilimia 38.2 wanatumia AI kutafuta mawazo mapya kulingana na taaluma zao.

Utafiti huo uliojumuisha sampuli ya wanafunzi 238 umebainisha kuwa zaidi ya robo tatu au asilimia 85.7 ya wanafunzi hutumia AI inayomilikiwa na kampuni ya Open AI ya Chatgtp, asilimia 41.1 hutumia QuillBot na asilimia 11.8 Grammarly.
Tofauti na miaka ya nyuma, utafiti huo unaeleza kuwa matumizi ya rejea kama vile vitabu na nukuu kutoka kwa wakufunzi vinatumika kwa uchache zaidi kwa asilimia 2.9 tu.
Matumizi ya AI kama nyenzo ya kujifunzia yamezua mjadala mpana ulimwenguni ikiwemo Tanzania huku baadhi wakisema ni jambo jema kwenda na teknolojia na wengine wakidai inaharibu wanafunzi.

Sehemu kubwa ya wakufunzi wanaona matumizi yaliyokithiri ya AI yanaathiri uwezo wa mwanafunzi kutafuta suluhu ya matatizo yanayomzunguka yakiwemo ya afya na uhandisi.
‘AI inazalisha kizazi kisicho na weledi’
Dk. Amin anasema kuwa nadharia pekee haifanyi wataaluma wa upasuaji kuwa wabobezi, jambo linalofanya kuwa na mipaka kwenye matumizi ya AI.
Taaluma ya upasuaji, Dk. Amin anaeleza kuwa inahitaji utendaji binafsi kwa kiasi kikubwa kitu ambacho hakiwezi kuletwa kwa wanafunzi wa taaluma hiyo kwa kutumia AI pekee.

“Hatuamasishi mwanafunzi kumezeshwa vitu na AI,” anaeleza Dk. Amin na kukazia kuwa hata upasuaji unaofanywa kwa roboti zilizopandikizwa AI bado unahitaji ukaribu sawa na upasuaji unaofanywa kwa mikono ya daktari.
Upasuaji unaofanywa na roboti unahitaji usimamizi zaidi kwa kuwa kinachofanyawa na AI kinaamriwa na daktari kifanyike na sio kwa kutegemea uwezo binafsi wa AI.
“Tutapata wapi tafiti mpya kama mwanafunzi ametumia AI kuandika tafiti,” amehoji Dk. Amin ambaye hakubaliani na matumizi makubwa wa AI kujifunzia masuala nyeti ya udaktari.
Wakati Dk. Amin akihofia matumizi ya AI kuzalisha wataalamu wasio na weledi kwenye taaluma hiyo nyeti inayogusa afya na uhai wa binadamu, Dk. Elisha Magolanga, Mkufunzi wa SJMC anasema matumizi ya AI katika taaluma ya elimu ya juu ni fursa.

“Hata Google ilipokuja watu walihofu tukaambiwa usikopi na kupesti lakini tukaitumia vizuri mpaka sasa,” anasema Dk. Magolanga akibainisha kuwa kila teknolojia na matokeo chanya na hasi.
Dk. Magolanga, anayesimamia masuala ya AI katika ndaki hiyo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema teknolojia ya AI imerahisisha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa nyenzo za kujisomea na uchakataji wa data mbalimbali, jambo linaloimarisha mchakato mzima wa kujifunza na kufundisha.
Wanafunzi wengi wanatumia AI bila kuelewa mipaka yake kimaadili na kitaaluma, anasema, kwa sababu ya ukosefu wa elimu sahihi juu ya matumizi bora ya teknolojia hiyo.

Matumizi makubwa ya AI ni hatari
Wataalamu wa saikolojia wanaonya kuwa matumizi yasiyo na mipaka yanaweza kuathiri kwa kina namna wanafunzi wanavyofikiri, kujifunza, na kujiamini katika kazi zao za kitaaluma.
Deo Sukambi, Mtaalamu wa Saikolojia, anasema kuwa matumizi ya AI kwa wanafunzi wa vyuo ni sawa na “kukwepa kazi ya ubongo”, jambo ambalo linazalisha kizazi cha watu wavivu wa kufikiri na wasio na uwezo wa kutatua changamoto kwa njia ya asili ya kiakili.

Tabia hiyo, anasema, inaweza kusababisha uraibu kwani akili ya binadamu huzoea kile inachofanyishwa mara kwa mara na ikiwa kazi nyingi zinafanywa kwa AI, basi uwezo wa kufikiri hufifia jambo ambalo linaweza kusababisha wanafunzi kutegemea teknolojia hiyo kupita kiasi hivyo kushindwa kufikiria njia mbadala wanapokumbana na matatizo.
“Unaweza kudhani unajirahisishia maisha sasa hivi lakini baadae maisha yako yakawa magumu sana,” anasema Sukambi.
Sukambi anawashauri wanafunzi kuzoea kutatua matatizo kwa kutumia akili zao wao wenyewe kwa kiasi kikubwa na si kwa kutegemea AI pekee.
Matumizi ya AI yanashika kasi vyuoni katika kipindi ambacho vyuo vikuu vinakosolewa kwa kuzalisha wahitimu wasiokuwa na ubora hitajika katika soko la ajira nchini.

Baadhi ya wakosoaji wanadai kuwa sehemu kubwa ya wahitimu wanakosa maarifa ya msingi ya kutatua matatizo madogo madogo kazini na kushindwa kuandika ripoti muhimu kazini.
Baadhi ya vyuo na vyuo vikuu vimeanza kuchukua hatua kuboresha matumizi yenye maadili ya AI ikiwemo kuboresha sera na miongozo kwa walimu na wanafunzi.
Profesa Baraka Maiseli, Mkuu wa Ndaki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CoICT) anasema kuna vyuo vichache Afrika Mashariki vyenye sera inayoongoza matumizi ya AI kwenye taaluma.
Mtaalamu huyo, anayesimamia uandaaji wa Sera na miongozo ya matumizi ya AI UDSM, anasema chuo hicho kimeshatoa sera inayoongoza matumizi sahihi ya AI kwa wanafunzi na wahadhiri.

“Walimu lazima wawe na ujuzi kuhusu AI kwa sababu wanafunzi wakati mwingine wanaweza kuwa wajanja wakatumia vibaya,” anasema Profesa Maiseli.
Serikali yaandaa Sera, miongozo
Uimarishaji wa matumizi sahihi ya AI yenye weledi si jukumu la vyuo vikuu pekee bali utashi wa Serikali kuhamasisha sera na miongozo namna ya kutumia vema teknolojia hiyo inayokua kwa kasi duniani.

Nukta Habari imefanya jitihada za kuwapata wasimamizi wa elimu Tanzania ikiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili kujua hatua wanazochukua kuhamasisha matumizi sahihi ya AI katika elimu ya juu bila mafanikio.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Adolf Faustine Mkenda, Serikali inaendelea kuandaa miongozo mbalimbali ya utoaji elimu na mafunzo nchini ili kuendana na matakwa ya Sera ya Elimu na Mafunzo ikiwemo matumizi ya AI katika Elimu.
Waziri Mkenda aliliambia Bunge Mei 2025 kuwa moja ya vipaumbele vya wizara yake ni kupeleka vijana sehemu mbalimbali nje ya nchi ili kujifunza ujuzi mbalimbali ikiwemo masuala ya teknolojia ya AI.

1 thought on “AI jinamizi lingine elimu ya juu Tanzania?”
Comments are closed.
Latest




AI ni mkombozi wa kurahisisha maisha ya kila siku sio tu katika taaluma bali katika kila hatua ya binadamu ila tu inabidi itumike kwa tahadhari na udhibiti wa hali ya juu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadae