Hatua kwa hatua jinsi kilimo cha mwani kinavyofanyika
- Njia maarufu ya kulima mwani ni kwa kutumia vigingi, ambapo vijiti huchomekwa chini ya maji na kamba hufungwa kati ya vigingi hivyo.
- Mbali na kutumika kama zao la biashara, mwani una matumizi mengine kwenye jamii.
Dar es Salaam. Huenda umeshawahi kusikia kuhusiana na zao la baharini liitwalo mwani.
Zao hili linalofanana na nyasi nyembamba na fupi huwa na rangi ya kijani, hudhurungi au nyekundu, humea au kupandwa baharini na hutumika kama chakula na viumbe wa baharini lakini pia huvunwa, kusindikwa na hutumiwa na binadamu kwa matumizi mbalimbali ikiwemo urembo au tiba.
Katika pwani ya Tanzania aina zinazolimwa zaidi ni Spinosum (mwekundu) na Euchema cotonii (gold).
Awali zao hili lilikuwa maarufu sana visiwani Zanzibar, lakini kwa sasa baadhi ya mikoa iliyopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi kama Dar es Salaam, Tanga pamoja na Mtwara nayo imeanza kuchangamkia fursa ya kilimo cha zao hilo.
Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mwani, Ripoti Shilika la Kimataifa la Maendeleo na Biashara (UNCTAD) ya Juni 2025 inaonyesha Tanzania iko kwenye orodha ya nchi kumi bora duniani kwa uzalishaji wa mwani, ikiwa na tani 167,400 kwa mwaka.
Wazalishaji wakuu wa mwani duniani ni China (tani milioni 22.4), Indonesia (tani milioni 9.2), Korea Kusini (tani milioni 1.7), Ufilipino (tani milioni 1.5), Japan (tani 309,400), Malaysia (tani 308,000), Urusi (tani 28,700) na Madagascar (tani 15,800).

Mwani aina ya Spinonus[mwani mwekundu] na Euchema cotonii [gold] ni mwani pekee unaolimwa sana nchini Tanzania hasa visiwa vya Zanzibar/Picha. Canva
Makala hii inaangazia mchakato wa kilimo cha mwani, ambapo Nukta Habari imezungumza na wakulima wa zao hilo kutokea Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Njia za kilimo cha mwani
Njia maarufu ya kulima mwani ni kwa kutumia vigingi, ambapo vijiti huchomekwa chini ya maji na kamba hufungwa kati ya vigingi hivyo.
Mbegu za mwani hufungwa kwenye kamba kwa kutumia taitai [ ni kamba za plastiki au ya katani inayoning’inizwa kwenye miundo ya mbao, miti au vigingi vilivyowekwa baharini ambapo vipandikizi vya mwani hufungwa ili vikue].
Njia nyingine ni njia ya chelezo, ambapo mbegu za mwani hufungwa kwenye mianzi iliyounganishwa na kuwekwa nanga, kisha kuelea karibu na uso wa maji.
Maandalizi ya shamba
Kabla ya kuanza kilimo, mkulima anatakiwa kuchagua eneo sahihi.
Jarida la Kilimo Endelevu Afrika Mashariki linaeleza kuwa eneo bora linapaswa kuwa na mchanga ili kurahisisha uchomekaji wa vigingi, lisilo na mawimbi makali na upepo, na pia maji yasikauke yote ili mwani usipigwe moja kwa moja na mionzi ya jua.
Kwa upande wake Mwanahawa Idd mkulima wa mwani kutoka Yaleyale Puna ameiambia Nukta Habari kuwa ni muhimu kuepuka eneo lenye tope kwa kuwa husababisha mwani kuharibika.
“Iwe sehemu yenye mchanga isiwe na mawe kwasababu eneo lenye mawe husababisha mti kushindwa kujihimili, lakini pia eneo lisiwe na tope ili kuepuka mwani kuharibika na kuoza,” amesema Idd.

Mara baada ya kupandwa, mwani huhitaji uangalizi wa karibu ili kuhakikisha kamba hazijakatika, kuondoa magugu ya baharini na kuzuia viumbe waharibifu. Picha l Canva
Jinsi ya kupanda mwani
Kwa mujibu wa Jarida la Better Management Practices[BMPs] la kilimo cha mwani Tanzania linaeleza kuwa, baada ya kuchagua eneo, mkulima huandaa vifaa muhimu ikiwa ni pamoja na kamba za nailoni au katani, vijiti vya miazi au mbao, pamoja na vipandikizi vya mwani.
Vipandikizi hivi hukatwa kutoka kwa mwani uliokomaa na kuwa na urefu wa sentimita 15 hadi 20.
Chapisho hilo linaeleza kuwa kuna mbinu kuu mbili za upandaji zinazotumika ambazo ni njia ya kamba chini ya bahari (off-bottom) na njia ya kamba zinazoelea juu ya maji (floating).
Katika njia ya kwanza, vijiti huwekwa ardhini chini ya maji, kamba hunyoshwa, na vipande vya mwani hufungwa kwa nafasi ya sentimita 20 hadi 30.
Katika njia ya pili, kamba hufungwa juu ya maji kwa msaada wa maboya au chupa za plastiki, na vipande vya mwani husalia vikining’inia kwenye uso wa bahari.
Mara baada ya kupandwa, mwani huhitaji uangalizi wa karibu. Kwa mujibu wa Mwanahawa Idd mkulima wa mwani kijiji cha Puna anasema kuwa shamba la mwani hukaguliwa kila mara ili kuhakikisha kamba hazijakatika, kuondoa magugu ya baharini na kuzuia viumbe waharibifu.

Kilimo cha mwani kimekuwa nguzo muhimu kwa wanawake wengi vijijini, kikiwa chanzo cha kujitegemea na kupunguza utegemezi majumbani. Picha l Sauda Ndaza/ Nukta Africa
Kwa kawaida, baada ya wiki sita hadi nane, mwani huwa tayari kwa kuvunwa. Baada ya kuvuna, huanikwa juani na kuuzwa kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Mwani unatakiwa uangalizi wa mara kwa mara hadi unapokuwa tayari kwa muda wa miezi miwili, unautoa baharini na kuuleta nchi kavu kwa ajiri ya kuanika, kisha unautoa kwenye kamba kuwa tayari kwa kuingia sokoni,” ameeleza Idd.
Faida za mwani
Mbali na kuwa zao la biashara, mwani una matumizi mengine muhimu kwenye jamii. Hutumika kutengeneza dawa ya mswaki, sabuni, barafu, chakula cha mifugo na hata keki.
Salma Saidi mkulima wa mwani kutoka Yaleyale, Kigamboni ameiambia Nukta Habari kuwa yeye huutumia mwani katika kuingiza kipato vilevile kutengeneza bidhaa kama mafuta pamoja na dawa ya tumbo.
“Kwanza napata pesa kwa kuuza, lakini pia mwani natumia katika kuchanganya na mafuta ya nazi ili kuweka mwili softi(laini) pia natumia kutengeneza dawa ya tumbo kwa kuchemsha na kunywa maji yake,” anasema Salma Saidi, mkulima kutoka Yaleyale Puna, Kigamboni.

Zao la mwani limekuwa maarufu hivi karibuni kutokana na Bidhaa zitokanazo na zao hili husaidia sana kwenye afya ya binaadamu/Picha google.
Changamoto za wakulima
Pamoja na mafanikio yake, wakulima hukumbana na changamoto kama vile upepo mkali ambao husababisha mwani kukatika kwenye kamba, pamoja na mvua kubwa zinasosababisha ugumu kukausha mwani na hivyo kuanza kuoza.
Wakulima wa Kijiji cha Puna wameiomba Serikali na wadau wa maendeleo wawasaidie kupata vifaa vya kisasa vya kuvuna na kusindika mwani jambo litakalowasaidia kuwaongezea kipato na kuboresha maisha yao.
Aidha, kilimo cha mwani kimekuwa nguzo muhimu kwa wanawake wengi vijijini, kikiwa chanzo cha kujitegemea na kupunguza utegemezi majumbani.
Hata hivyo, ili kuwasaidia wakulima wa mwani kuongeza kiwango cha uzalishaji na ubora wa mwani katika soko la ndani na nje ya nchi Serikali inatoa mafunzo kwa vikundi vya wakulima jinsi ya kutumia vifaa mbalimbali vya kutengenezea bidhaa kama vile vifungashio vya bidhaa.
Mafunzo hayo hutolewa kwenye vikundi vya kilimo cha mwani ili kuvijengea uwezo wa kilimo bora, usimamizi wa vikundi, usimamizi wa fedha,utunzaji kumbukumbu, kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao pamoja na masoko ya zao la mwani ambapo kwa sasa yanafanyika kwa vikundi vya wanawake na vijana vya wakulima wa zao hilo Wilaya ya Mkinga, Mkoani Tanga.
Huratibiwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kushirikiana na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kwa ufadhili wa Serikali ya Japan pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Latest