Viongozi mashuhuri, taasisi wanavyoomboleza kifo cha Job Ndugai
Dar es Salaam. Taifa la Tanzania linaomboleza kifo cha Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania na aliyekuwa mbunge wa Kongwa Job Yustino Ndugai kilichotokea jana Agosti 6, 2025 jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Spika wa Bunge Tulia Ackson iliyotolewa jana majira ya saa 12 jioni Ndugai amefariki akiwa na umri wa miaka 62.
Salamu za rambirambi zinaendelea kutolewa na taasisi na watu mashuhuri ikiwemo viongozi wa kisiasa wakimuomboleza kiongozi huyo ambaye kifo chake kimetokea siku mbili tu baada ya kuongoza katika kura za maoni za kukiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea ubunge wa jimbo la Kongwa.
Mara baada ya taarifa za kifo kutangazwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii alisema amepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Ndugai na ametoa pole kwa familia, wanachama wote wa CCM, watumishi wa Bunge na wabunge wote aliotumikia nao akiwa Spika wa Bunge la Tanzania, wananchi wa Kongwa, ndugu jamaa na marafiki.
Rais Samia ametoa wito kwa Watanzania kuungana pamoja na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu na kuiombea familia, ndugu, jamaa na marafiki uvumilivu, faraja na moyo wa ibada katika kipindi hiki kigumu.
Spika wa Bunge Tulia Ackson nae ameungana na Rais Samia kutoa salamu za rambirambi na kumuombea pumziko la amani bosi wake huyo wa zamani na mshauri wake.
Aidha, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa naye leo Agosti 7, amechapisha katika kurasa zake za mitandao ya kijamii salamu za rambirambi ambapo amewaombea kwa Mwenyezi Mungu utulivu familia ya Ndugai, Wakazi wa Kongwa, wanafamilia wa Bunge la Tanzania katika kipindi cha maombolezo.
Kwa upande wake kiongozi mstaafu wa Chama Cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe, kupitia ukurasa wake wa X zamani Twitter ameandika “natoa salamu za pole kwa familia na wananchi wa Kongwa kwa msiba huu mkubwa, Mungu aiweke roho yake mahala pema peponi Amina.”
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) navyo vimeeleza kupokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Ndugai na kutoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, wananchi wa Kongwa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo.
Kwa sasa kinachosubiriwa ni ratiba ya msiba huo wa kiserikali ambayo huenda ikaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Bunge.
Kwa upande wako utamkumbuka kwa lipi spika mstaafu Job Ndugai, tuandikie kwenye maoni?