Ndugai afariki dunia leo Agosti 6, 2025
- Tulia atoa pole kwa familia, asema Taifa limepoteza kiongozi muhimu na mwanasiasa mkongwe.
Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Yustino Ndugai, amefariki dunia leo Agosti 6, 2025, jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson, Ndugai amefariki dunia akiwa jijini Dodoma ingawa sababu za kifo chake bado hazijawekwa wazi.
Dk. Tulia ametoa pole kwa familia na kueleza kuwa Taifa limepoteza kiongozi muhimu, mwanasiasa mkongwe na Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania.
“Natoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa Jimbo la Kongwa. Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” amesema Dk. Tulia kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma cha Bunge la Tanzania.

Aidha, kwa upande wake Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, pia ameungana na watanzania kuomboleza kifo hicho kwa kutuma salamu za pole na kuwataka Watanzania kuungana katika kumuombea marehemu na kuwaombea wafiwa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninatoa pole kwa familia, wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi, watumishi wa Bunge na Wabunge wote aliotumikia nao akiwa Spika wa Bunge letu, wananchi wa Kongwa, ndugu, jamaa na marafiki.” ameandika Rais Samia.
Job Yustino Ndugai alizaliwa Januari 22, 1963, na alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kongwa kwa miaka kadhaa kabla ya kuchaguliwa kuwa Naibu Spika mwaka 2010. Baadaye alihudumu kama Spika wa Bunge kuanzia mwaka 2015 hadi alipojiuzulu Januari 2022.
Alichukuliwa kuwa mmoja wa viongozi waliotoa mchango mkubwa katika kuimarisha taasisi ya Bunge nchini, akiwa na historia ya utumishi uliotukuka, nidhamu ya hali ya juu na uongozi uliozingatia sheria na taratibu.
Itakumbukwa pia kuwa hivi karibuni, Ndugai alishinda katika kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Kongwa, hatua iliyomuweka katika nafasi nzuri ya kurejea bungeni kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Kamati ya Mazishi pamoja na familia ya marehemu inaratibu mipango ya maziko na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa kadri maandalizi yanavyofanyika.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.