INEC: Watendaji uchaguzi epukeni kuwa chanzo cha migogoro
- Tume yasisitiza usawa, ushirikishwaji na kuzingatia mabadiliko ya sheria mpya ya uchaguzi
Mwanza. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka watendaji wake kujiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha migogoro au malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi, na badala yake wahakikishe wanazingatia sheria, kanuni na miongozo yote ya tume katika utendaji wao.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 21, 2025 jijini Mwanza na Mjumbe wa Tume hiyo, Jaji Asina Omari, wakati akiwaapisha watendaji wa uchaguzi 110 kutoka mikoa ya Mwanza na Mara.
Watendaji hao ni pamoja na waratibu wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, maofisa wa uchaguzi na maafisa manunuzi.
Akitoa maelekezo maalum, Jaji Asina amewataka watendaji hao kuondokana na mazoea na kuzingatia kuwa mazingira ya uchaguzi yamebadilika, hususan baada ya kuanza kutumika kwa sheria mpya ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
“Vishirikisheni vyama vyote vyenye usajili kamili katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi, kulingana na matakwa ya Katiba, sheria na maelekezo ya tume,” amesema Jaji Asina.
Aidha, amewasisitiza kuhakikisha ushirikishwaji wa wadau wa uchaguzi, hasa katika maeneo yanayohitaji usimamizi wa karibu kwa mujibu wa sheria na maelekezo ya tume.
Pia, amewataka kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema, huku wakihakikisha vinapangwa kwa kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Watendaji hao ni pamoja na waratibu wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, maofisa wa uchaguzi na maafisa manunuzi. Picha l INEC
Majina ya wasimamizi sasa wazi kwa umma
Kwa upande wake, Wanchoke Chinchibera, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ukerewe, amesema hatua ya kuchapisha majina ya wasimamizi kwenye gazeti la Serikali ni ya kihistoria na inaleta uwazi mkubwa katika mchakato wa uchaguzi.
“Tofauti na zamani, sasa majina ya wasimamizi wa majimbo yako hadharani, hali hii itaondoa malalamiko yaliyokuwa yakijitokeza awali na hivyo kuufanya uchaguzi kuwa huru na haki,” amesema Chinchibera.
Naye Mohamed Chade, Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Magu, amesema baada ya mafunzo hayo, watendaji wamejipanga kuhakikisha kuwa kila kundi la jamii linaheshimiwa na kwamba uchaguzi unasimamiwa kwa haki na usawa.
“Tutaenda kutekeleza wajibu wetu kwa kuzingatia haki, na kuhakikisha hakuna kundi linalonyimwa nafasi. Lengo ni kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa wa haki na wenye ushirikishwaji wa kweli,” amesema Chade.
Kauli hizi zinakuja wakati nchi ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu mwezi Oktoba 2025, ambapo wadau wengi wamekuwa wakihimiza tume kuhakikisha chaguzi zinakuwa huru, haki na zenye kuwajumuisha watu wote, wakiwemo wenye ulemavu na wanawake.
Latest