Rais Samia: legezeni masharti utoaji mikopo ya 10%
- Ataka waombaji wasaidiwe kujaza fomu za uombaji mikopo.
- Awataka waliopata mikopo hiyo kufanya marejesho kwa wakati.
Dar es salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa halmashauri nchini kulegeza masharti na vigezo vya kupata mikopo inayotolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili kutimiza lengo lililokusudiwa la kuyakwamua makundi hayo kiuchumi.
Mikopo hiyo inatokana na asilimia 10 za mapato ya ndani ya kila halmashauri nchini ambayo hutolewa kwa vikundi au mtu mmoja mmoja kutegemeana na vigezo vilivyowekwa.
Rais Samia aliyekuwa akihutubia wananchi wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu ameeleza kuwa baadhi ya vijana wanashindwa kupata mikopo hiyo kutokana na kushindwa kutekeleza masharti yaliyowekwa ikiwemo kushindwa kujaza fomu ya mkopo kwa usahihi.
“Kuna watu wanahitaji mikopo hii yale mafomu mliyowawekea wanashindwa kujaza vilivyo, mnapofanya tathmini mnasema hawa hawakujaza vizuri wasipewe, lakini kumbe ndio wenye haja ya hizo pesa, naomba mlegeze masharti na muwasaidie,” amesema Rais Samia.

Hata hivyo, pamoja na kutaka masharti ya utoaji mikopo yalegezwe Rais Samia amewataka waliopatiwa mikopo kufanya marejesho kwa wakati ambapo amewaomba madiwani kusimamia zoezi hilo ili kutoa nafasi kwa wengine kupata.
Itakumbukwa kuwa Rais Samia alisitisha utoaji wa mikopo hiyo mwaka 2023 mara baada ya kubainika kwa mapungufu ikiwemo pesa kutolewa kwa vikundi hewa na kutorejesha madeni kwa wakati jambo lililoisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh80 bilioni.
Serikali ilitangaza kuanza kutoa tena fedha hizo Julai Mosi mwaka 2024 mara baada ya kufanyia maboresho mapungufu yaliyokuwepo ikiwemo uanzishwaji wa kamati za usimamizi wa mikopo katika ngazi za ofisi za wakuu wa mikoa, halmashauri na kata.
Rais Samia anayehitimisha ziara yake mkoani humo ametumia nafasi hiyo kuwasisitiza wafanyabiashara wadogo kulipa kodi kwa maendeleo ya halmashauri zao na Taifa kwa ujumla.
Mkuu huyo wa nchi ametoa tahadhari kuwa iwapo wananchi hawatolipa kodi huenda hali ikawa ngumu kufuatia migogoro ya kisiasa inayoendelea katika maeneo mbalimbali ikiwemo vita kati ya Iran na Israel.
“Wanakopigana kule madhara yanakuja kwetu, tutasikia bei za mafuta zimepanda…kwa sababu wale ndio wenye nguvu walioshikilia soko la dunia,” ametahadharisha Rais Samia.
Rais Samia mara baada ya kutimiza siku za ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu anatarajia kuelekea mkoani Mwanza ambapo pamoja na mambo mengine atazindua daraja la Magufuli kesho Juni 19, 2025.
Latest



