Spika Tulia ataka majibu ya Serikali tuhuma matumizi mabaya ya fedha Arusha.
- Ni tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo.
- Asema kuna watumishi wanashirikiana kufanya ubadhirifu wa fedha hizo.
- Waziri aahidi kuwasilisha taarifa akihitimisha maombi ya bajeti ya wizara yake.
Dar es salaam. Spika wa Bunge la Tanzania Tulia Ackson amemuagiza Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mohamed Mchengerwa kuandaa taarifa ya ufafanuzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha mkoani Arusha zilizoibuliwa na Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo.
Gambo ameibua tuhuma hizo leo Aprili 16, 2025 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha mchango wake wa bajeti ya Tamisemi ya mwaka 2025/26 ambapo amesema kuna matumizi mabaya ya fedha katika ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Jiji la Arusha, akidai kuwepo kwa upotoshaji wa vipimo na ongezeko la gharama kinyume na makubaliano ya mkataba.
“Katika jengo la utawala, gharama zake za jumla hazipungui bilioni 9. Jengo la ghorofa nane unalijenga kwa bilioni tisa, maana yake kila ghorofa moja ni zaidi ya bilioni moja…juzi wameingia mkataba wa Sh6.2 bilioni, lakini baadhi ya vipimo vilivyoandikwa kwenye BOQ ‘Bill of Quantities’ na utekelezaji wake ni tofauti.” amesema Gambo.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, moja ya kasoro alizozibaini ni pamoja na mlinganyo wa vipimo uliosababisha ongezeko la gharama ya Sh252 milioni, pamoja na tofauti nyingine ya vipimo iliyosababisha mkataba huo kuwa na ongezeko la takribani Sh1.5 bilioni zaidi ya gharama halisi.
“Gharama halisi zilitakiwa kuwa bilioni 3.4, lakini wameingia mkataba wa bilioni 6.2, kuna ziada ya zaidi ya bilioni 2.8,” amesisitiza Gambo.

Mbunge huyo ameenda mbali zaidi kwa kumtaka Waziri wa Tamisemi kuongeza umakini na usimamizi wa karibu kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akidai kuna mtandao wa baadhi ya watumishi wa umma wanaoshirikiana kutumia vibaya fedha za serikali.
“Na wanashirikiana ni ‘teamwork’, wanashirikiana katika kulimaliza Jiji la Arusha,” amesema Gambo kwa msisitizo.
Kufuatia tuhuma hizo, Spika wa Bunge la Tanzania, Tulia Ackson, amemuagiza Waziri Mchengerwa kuandaa taarifa fupi kuhusu ujenzi wa jengo hilo na kuwasilisha bungeni mara baada ya mjadala wa bajeti ya wizara hiyo kukamilika.
“Kwa uzito wa tuhuma hizi, Mheshimiwa Waziri, tunapomaliza bajeti yako, tunaomba utuletee taarifa ndogo ya ujenzi wa hilo jengo. Kwa sababu tuhuma zimetolewa hapa bungeni, tukimaliza kujibu tutajua bunge lichukue hatua gani,” amesema Spika Ackson.
Kwa upande wake Waziri Mchengerwa amekiri kupokea agizo hilo na kuahidi kuiwasilisha atakapokuwa anahitimisha maombi ya bajeti ya wizara yake Aprili 22, mwaka huu.
Latest



