Rais Samia apitisha miswada saba kuwa sheria
- Ni pamoja na Mswada wa Sheria wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wa mwaka 2024.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amepitisha miswada saba iliyopitishwa na Bunge katika Mkutano wa 18 wa Bunge la 12 kuwa sheria rasmi za nchi, hatua inayolenga kuimarisha utendaji wa taasisi mbalimbali na kuboresha huduma kwa wananchi.
Akiwasilisha taarifa ya Spika kuhusu kazi zilizokamilika katika mkutano uliopita, leo Aprili 8, 2025 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 19 wa Bunge, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu ameliarifu Bunge kuwa tayari miswada hiyo saba imesainiwa na Rais na sasa inatambuliwa rasmi kama sheria.
“Napenda kuliarifu Bunge hili tukufu kuwa miswada hiyo saba imepata kibali cha mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa sheria za nchi” amesema Zungu.
Moja ya miswada iliyopitishwa na kusainiwa kuwa sheria ni pamoja na Mswada wa Sheria wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wa Mwaka 2024 uliolenga kuliwezesha shirika hilo kukabiliana na changamoto za kifedha, kiutendaji, na kiteknolojia ambazo zimekuwa zikilikabili kwa miaka mingi.
Muswada huo ambao kwa sasa ni sheria unaipa TBC msingi thabiti wa kisheria na kuiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa kuzingatia mahitaji ya kisasa na mabadiliko ya teknolojia.
Kwa mujibu wa maelezo aliyoyatoa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi, kabla muswada huo haujapitishwa na kuwa sheria alisema kuwa sheria hiyo itatambua TBC kama shirika muhimu la umma linalohusika na utangazaji wa habari, burudani, na elimu.
Pia itaipa mamlaka ya kusimamia rasilimali zake na kuhakikisha kuwa inaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Miswada mingine iliyopitishwa na kuwa sheria ni pamoja na Mswada wa Sheria wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 3 wa Mwaka 2024, Mswada wa Sheria wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 4 wa Mwaka 2024, Mswada wa Sheria wa Marekebisho ya Sheria za Kazi wa Mwaka 2024, Mswada wa Sheria wa Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira wa Mwaka 2024, Mswada wa Sheria wa Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi wa Mwaka 2024, na Mswada wa Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Nyongeza ya Fedha za Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Upitishwaji wa miswada hiyo saba unatarajiwa kuleta tija kubwa kwa taifa kwa ujumla. Sheria mpya na zilizoboreshwa zitasaidia kuimarisha mazingira ya kazi, kulinda mazingira, kuvutia uwekezaji zaidi kupitia maeneo maalum ya kiuchumi, na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.
Latest



