Rais Samia afanya uteuzi wa viongozi na kuwapangia mabalozi vituo vya kazi
- Ateua viongozi watatu na mabalozi wawili wa kuiwakilisha Tanzania nchini Msumbiji na Sweden.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali pamoja na kuwapangia vituo vya kazi Mabalozi wa Tanzania katika mataifa tofauti.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Dk Moses Kusiluka, iliyotolewa Machi 25, 2025 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu Pemba imewataja viongozi walioteuliwa kuwa ni pamoja na Rachel Stephen Kasanda ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi.
Nafasi hiyo ya Kasanda awali ilikuwa ikishikiliwa na Lauteri John Kanoni ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Viongozi wengie walioteuliwa ni Prof Jafari Ramadhani Kideghesho aliyeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania, ambapo anatarajiwa kuimarisha usimamizi wa rasilimali za wanyamapori nchini.
Kwa upande wa CPA Ashraph Yusuph Abdulkarim ameteuliwa kuwa Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo, shirika muhimu kwa uchumi wa nchi.
Katika nyanja za kidiplomasia, Balozi Hamad Khamis Hamad amepangiwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, huku Balozi Mobhare Holmes Matinyi akipangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden.
Uteuzi huu huenda unalenga kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na mataifa hayo, hususan katika masuala ya kiuchumi na kidiplomasia.
Latest



