Zaidi ya nusu ya wakazi Arusha hawana maji safi

March 14, 2025 5:40 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Upatikanaji wa maji safi jijini Arusha umeongezeka hadi asilimia 99, kutoka asilimia 68 zilizokuwepo awali.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA), Mhandisi Justine Rujomba, amesema ndani ya miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita wamefanikiwa kufikisha maji safi na salama kwa watu zaidi ya milioni 1 jijini humo.

Rujomba aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Machi 13, 2025 jijini Dodoma amesema kuwa mamlaka hiyo imefanikiwa kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji safi kutoka lita milioni 40 hadi lita milioni 200 kwa siku yakinufaisha zaidi ya watu milioni 1 wa jiji hilo,

“Zaidi ya watu milioni 1 sasa wanufaika na huduma ya maji kutoka watu 400,000 Serikali ikiwezesha upatikanaji wa magari mawili ya usambazaji wa maji safi kwa ajili ya kutoa huduma sehemu ambazo bado mtandao wa maji safi haujafika,” amesema Rujomba.

Licha ya mafanikio hayo ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan bado zaidi ya nusu ya wakazi wa jiji hilo hawana huduma hiyo huku ikisalia miezi miezi michache kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Jiji hilo lina watu milioni 2.4 hivyo zaidi ya wakazi milioni 1.4 hawana huduma ya maji safi na salama na kufanya baadhi yao kutumia vyombo vya habari na majukwaa ya mtandaoni kuelezea shida ya upatikanaji huo wa maji.

Novemba 12, 2024 tovuti ya habari ya Mwananchi liliripoti ukosefu wa maji katika Kijiji cha Oltepes, kilichopo Kata ya Orbomba, wilayani Longido, uliosababisha wanawake wa kijiji hicho kutumia mkojo kujihifadhi wakiwa hedhi.

Si wakazi wa vijijini tu wanaokumbana na shida hiyo ya maji, Februari 15 mwaka huu mmoja wa watumiaji wa jukwaa maarufu la Jamii Forums alilalamikia ukosefu wa maji kwa siku hadi tatu huku mkazi mkazi mwingine Sombetini jijini humo akilalamikia maji hayo kutoka machafu kiwango ambacho hakikidhi mahitaji.

Kutokana na malalamiko hayo, Serikali ilijitokeza mara kadhaa ikiahidi kuzishughulikia na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama katika jiji hilo.

Mafanikio mengine yaliyotajwa ni ujenzi wa mabwawa 18 yenye uwezo wa kutibu lita milioni 22 kwa siku, huku mabwawa ya zamani yakiwa na uwezo wa kutibu lita milioni 3.5 kwa siku. 

Hii inafanya jiji la Arusha kuwa kinara nchini kwa kuwa na mtambo mzuri wa kutibu maji safi na salama, na kiwango cha ongezeko kikiwa asilimia 39.5, kutoka asilimia 7.6 awali.

“Kwa sasa, upatikanaji wa maji safi jijini Arusha umeongezeka hadi asilimia 99, kutoka asilimia 68, na mahitaji ya maji kwa jiji na maeneo yanayohudumiwa ni lita milioni 139,” ameeleza Rujomba.

Uzalishaji wa maji umefikia lita milioni 200, hali inayosababisha kuwepo kwa maji ya ziada.

Pamoja na hayo, mamlaka hiyo imeendelea kutoa huduma kwa wafugaji kwa kujenga mabwawa katika maeneo ya Longido, Monduli na Ngorongoro kwa ajili ya kunyweshea mifugo na kuboresha ustawi wa mifugo katika maeneo hayo. 

Rujomba ameongeza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji safi na usafi wa mazingira wenye thamani ya Sh520 bilioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks