Tanzania yapanga kukusanya na kutumia Sh57 trilioni bajeti ya Serikali 2025/26
- Bajeti yaongezeka kwa asilimia 14 kulinganisha na ya mwaka wa fedha unaokaribia kuisha.
Arusha. Serikali ya Tanzania imepanga kukusanya na kutumia Sh 57.4 trilioni katika mwaka wa fedha 2025/ 26 huku kiasi kikubwa cha fedha kikielekezwa kukamilisha miradi ya maendeleo
Taarifa hiyo ya Serikali inakuja ikiwa imesalia miezi mitatu kumaliza mwaka wa fedha 2024/25 na kuanza kwa mwaka mpya wa fedha Julai mosi mwaka huu.
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba aliyekuwa akiwasilisha mpango wa mapato na matumizi wa mwaka 2025/26 Machi 11, 2025 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Bunge la Bajeti linalotarajiwa kuanza April mwaka huu.
Mwigulu alibainisha kuwa fedha hizo ni ongezeko la asilimia 13.4 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha unaokaribia kuisha.
Itakumbukwa kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/25 Serikali ilitenga ShSh49.35 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge la Tanzania kama bajeti ya Serikali kuu na baadae kuongeza Sh945.7 bilioni Februari mwaka huu na kufanya kufikia Sh50.4 trilioni.
Endapo bajeti hiyo mpya iliyoongezeka kwa Sh7 trilioni likipitishwa na Bunge, Tanzania itakuwa imeongeza zaidi ya Sh21trilioni katika bajeti ya Serikali kuu tangu kuingia kwa Rais Samia madarakani.

Baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali wakisiliza wasilisho la mpango wa mapato na matumizi wa mwaka 2025/26 .Picha|Wizara ya Fedha.
Hata hivyo, huenda ongezeko hilo la bajeti linatokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo aliyoirithi kwa mtangulizi wake ikiwemo bwawa la kufua umeme la Mwalimu Julius Nyerere na ujenzi wa reli ya a kisasa inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi na pato la Taifa.
Ndani ya miaka hiyo minne pia Tanzania imerekodi kupanda na kushuka kwa uchumi tangu kutokea kwa janga la janga la Uviko 19 mwaka 2019 na 2020.
Mwaka 2021 Tanzania ilirekodi ukuaji wa uchumi wa asilimia 4.8 iliyoshuka hadi asilimia 4.7 mwaka 2022 na baadae kuongezeka hadi asilimia 5.1 mwaka 2023, mwaka 2024 uliongezeka tena hadi asilimia 5.4 ukitarajiwa kuongezeka zaidi mwaka huu.
“Shabaha za uchumi kwa mwaka 2025/2026, ni kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kufikia asilimia 6.0 kutoka matarajio ya asilimia 5.4 mwaka 2024, mapato ya ndani yanatarajiwa kufikia asilimia 16.4 ya Pato la Taifa mwaka 2025/2026, ikilinganishwa na asilimia 15.8 inayotarajiwa kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025,” alisema Dk Mwingulu.
Dk Mwigulu ametaja maeneo yaliyotengewa fedha katika bajeti ya 2025/26 kuwa ni, maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), mwaka 2027, ambapo Tanzania itashirikiana na nchi jirani kuandaa.
Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, akiwasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2025/2026 ambapo alisema kuwa vipaumbele vilivyopendekezwa vimezingatia malengo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano.
Latest



