CCM yatangaza ukomo wa wabunge wa viti maalum
- Wabunge wa viti maalum kuhudumu kwa miaka 10.
- Utaratibu huo utaanza kutumika mwaka 2030.
Arusha. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza ukomo wa na nafasi ya ubunge, uwakilishi na udiwani wa viti maalum kuwa ni miaka 10.
Viti maalumu no utaratibu uliowekwa na Serikali ya Tanzania mwaka 1995 kwa nafasi za ubunge na udiwani kama njia ya kuwajengea uwezo wanawake na kuondoa tofauti kubwa ya uwakilishi kati ya wanaume na wanawake katika vyombo vya maamuzi.
Taarifa ya CCM iliyotolewa leo Machi 11, 2025 inabainisha kuwa uamuzi huo umetokana na kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, kilichofanyika jana Machi 10 kikijadili ajenda mbalimbali ikiwemo ukomo wa wabunge, madiwani na wawakilishi hao.
“Kuweka ukomo wa vipindi viwili vya miaka mitano kwa nafasi za ubunge/uwakilishi na udiwani wa viti maalum wanawake. Ukomo huo utaanza kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030,” imesema taarifa ya CCM.
Taarifa hiyo imekuja wakati ambao Tanzania inaelekea kweye Uchaguzi Mkuu wa Rais Wabunge na Madiwani huku kikiwa na maoni lukuki kuhusu ukomo wa wabunge na madiwani hao kutoka kwa wanasiasa wa upinzani na baadhi ya viongozi wastaafu.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais Tanzania Samia Suluhu Hassan akiongoza Kikao cha Kawaida cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika Mkoani Dodoma tarehe 10 Machi, 2025.Picha |CCM.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, akizungumza na vyombo vya habari kwa nyakati mbalimbali alionesha umuhimu wa chama chake na Serikali kutangaza ukomo huo ili kutoa nafasi kwa watu wengine kushika hatamu ya uongozi.
Hata alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho mapema Januri mwaka huu Lissu hakusita kutangaza msimamo wakeakiahidi i kubadili mfumo wa viti maalum vya udiwani na ubunge kwa wanawake ndani ya chama hicho.
Pamoja na Lissu viongozi wengine waliowahi kutoa maoni husiana na ukomo wa nafasi hiyo ni pamoja na Zakia Meghji, aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha, aliyetaka ubunge huo uwe na ukomo wa miaka miwili kama ilivyo kwa nafasi ya Rais.
Megji alitoa maoni hayo alipokuwa akizungumza kwenye kongamano la wanawake na uongozi lililofanyika Disemba , 2024 jijini Dar es Salaam , Meghji alisema kuwa ukomo huo utapunguza upendeleo na viashiria vya rushwa.
Aidha, CCM imetangaza imepitisha Kauli Mbiu rasmi kwa ajili ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 isemayo kazi na utu tunasonga mbele ikilenga kuendeleza juhudi za ujenzi wa Taifa.
“Kauli mbiu hiyo inaakisi dhamira ya Chama ya kuendeleza juhudi za ujenzi wa Taifa lenye maendeleo jumuishi, mshikamano wa kitaifa na ustawi wa watu wenye kujali utu,” imesema taarifa ya CCM
Latest



