Rais Samia: Mnaotaka kugombea ubunge, udiwani toeni taarifa mapema
- Ni kwa ajili ya Serikali kutatayarisha watu wa kushika nafasi hizo kwa kuwapa miongozo na mafunzo yanayohitajika katika nafasi husika.
- Asema kiongozi atakayegombea bila kutoa taarifa mapema hatapata nafasi zote za uongozi.
Dar es salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa ikiwemo wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na wa mikoa kutoa taarifa mapema kama wana mpango wa kugombea ubunge ili nafasi zao zijazwe mapema na watu wenye sifa huku akiwaonya kutoshitukiza wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo Jumanne Machi 11, 2025 jijini Dodoma katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa 39 wa viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat) amewaambia wahudhuriaji kiongozi atakayegombea bila kutoa taarifa mapema hatapata nafasi zote za uongozi.
“Yeyote mwenye nia ya kugombea atuambie mapema ili tumpandishe wa chini yake ashike ile nafasi, hatutaki pale wakati fomu zinatoka watu wote wanakimbia kwenda kuzichukua na mnatuacha Serikali za Mitaa hatuna viongozi, hazina wasimamizi, mnabakia kujaza watu ambao hawana experience (uzoefu),” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameongeza kuwa kwa kupata taarifa mapema Serikali itatayarisha watu wa kushika nafasi hizo kwa kuwapa miongozo na mafunzo yanayohitajika katika nafasi husika.
“Sasa usipojisema mapema, ukaja kuchukua fomu mbele umekosa yote, umekosa fomu umekosa cheo, nafasi yako utaiacha, ukituambia mapema, umekwend kujaribu, umeshindwa na wewe ni mzuri tutakufikiria kurudi,” amesisitiza Rais Samia.
Rais Samia anatoa kauli hiyo ikiwa imesalia miezi saba kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu ambapo baadhi ya viongozi kwenye nafasi za kuteuliwa katika mamlaka za Serikali za Mitaa huzikacha nafasi zao na kwenda kuwania nafasi za ubunge au udiwani.
Uchaguzi wa mwaka 2020 ulishuhudia baadhi ya wateule wa Rais kwenye nyadhifa mbalimbali akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda aliyetia nia kugombea Jimbo la Kigamboni n kisha kuenguliwa kwenye nafasi hiyo na Rais wa awamu ya tano John Magufuli.
Aidha, Rais Samia amewasisitiza viongozi wa halmashauri kufuata sheria na taratibu wanapositisha uwekezaji katika maeneo yao ya kiutawala ilikuepusha faini zinazolipwa na Serikali baada ya wawekezaji kupeleka kesi katika mahakama za kimataifa na kushinda.
Latest



