Ripoti: Tanzania yapanda viwango mapambano dhidi ya rushwa

March 4, 2025 3:39 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mwaka 2024 mapambano dhidi ya rushwa yalifikia asilimia 41..
  • Tanzania yashika nafasi ya 82 kati ya 180 kwa viwango vya rushwa.

Arusha. Huenda vitendo vya rushwa vikazidi kupungua nchini Tanzania mara baada ya ripoti mpya ya kuonesha kuongezeka kwa viwango vya mapambano dhidi ya rushwa kwa miaka miwili mfululizo.

Ripoti hiyo inayotolewa na Taasisi ya Transparent International inaonesha viwango vya mapambano dhidi ya rushwa vimefikia asilimia 41 ya 100 mwaka 2024 kutoka asilimia 40 iliyorekodiwa mwaka 2023.

Matokeo hayo ni kulingana na kiashiria cha ‘Corruption Perception Index (CPI)’ kilichoanzishwa mwaka 1995 kwa lengo la kupima hali ya rushwa katika nchi mbalimbali duniani ambapo kadri nchi inavyopata alama kubwa huashiria kuwa viwango vya rushwa ni vya chini.

Viwango hivyo vinaonesha jinsi Tanzania inavyopiga hatua kila mwaka katika mapambano dhidi ya rushwa ikipanda na kushuka kwa miaka tofauti ndani ya miaka 10.

“Alama ya nchi (country’s corruption score) inaonyesha mtazamo wa kiwango cha rushwa katika sekta ya umma kwa skala ya 0 hadi 100, ambapo 0 inaashiria rushwa iliyokithiri na 100 inaashiria nchi isiyo na rushwa kabisa,” imesema ripoti hiyo.

Kwa miaka mingi, Tanzania imekuwa ikipambana na vitendo vya rushwa kupitia jitihada mbalimbali, ikiwemo kuimarisha taasisi za kupambana na rushwa, kutunga sheria madhubuti, na kuongeza uwazi katika utoaji wa huduma za umma.

Mbali na jitihada hizo, viongozi mbalimbali wakitaifa wamekuwa wakikemea hadharani vitendo vya rushwa akiwemo Rias Samia Suluhu Hassan ambaye amenukuliwa mara kadhaa akikemea vitendo hivyo kutokana na madhara yanayolisababishia taifa.

“Tanzania si kichaka cha kuficha fedha za rushwa na wala si salama kwa  wala rushwa,” alisema Rais Samia Julai 11,2023 katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Rushwa  Afrika yaliyofanyika jijini Arusha.

Kwa mujibu wa Global international vyanzo vya takwimu vilivyotumika kufanya tathmini hiyo ni pamoja na, uelekezaji mbaya wa fedha za umma, Uwezo wa serikali kudhibiti ufisadi katika sekta ya umma, Maafisa wa umma kutumia madaraka yao kwa manufaa binafsi, urasimu na uteuzi wa upendeleo katika utumishi wa umma.

Hata hivyo, utafiti huo haukuhusisha masuala kama mtazamo wa moja kwa moja wa wananchi au uzoefu wao kuhusu ufisadi, ulaghai wa kodi, mtiririko haramu wa fedha, wasaidizi wa ufisadi kama wanasheria, wahasibu, na washauri wa kifedha, utakatishaji wa fedha, ufisadi katika sekta binafsi, chumi usio rasmi na masoko yasiyo rasmi

Tathmini hizo za rushwa zilipimwa kwa kutumia mchanganyiko wa angalau vyanzo vitatu vya takwimu vilivyotolewa kutoka tafiti na tathmini 13 tofauti za rushwa. 

Vyanzo hivi vya takwimu vinakusanywa na taasisi mbalimbali zinazotambulika, ikiwemo Benki ya Dunia (WB) na Jukwaa la Uchumi la Dunia.

Pamoja na viwango hiyo, ripoti hiyo imebainisha kuwa nchi ya Tanzania imeshika nafasi ya 82 katika mapambano dhidi ya rushwa kati ya nchi 180 zilizofanyiwa tathimini.

Tanzania imeshika nafasi sawa na nchi nyingine za Afrika ikiwemo Burkina Faso na Afrika Kusini ambazo nazo zimeshika nafasi ya 82 ambazo viwango vyake havijaongezeka kwa mwaka 2024

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks