Ifahamu eSim, faida na changamoto zake

February 7, 2025 4:44 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni teknolojia inayokuwezesha kutumia mtandao bila kuweka laini ya simu.
  • Hupunguza hatari ya kupoteza taarifa muhimu kwa kupoteza au kuibiwa laini ya simu.

Dar es Salaam. Teknolojia ya mawasiliano inaendelea kupiga hatua kubwa tangu uvumbuzi wa kadi za SIM miaka ya 1990. 

SIM ni kifupi cha Subscriber Identity Module, ambayo ni kadi maalum inayotumika kuhifadhi taarifa za mtumiaji wa mtandao wa simu, ikiwa ni pamoja na namba ya simu, mawasiliano, na hati za utambulisho za mtandao.

SIM inaruhusu simu kuunganishwa na mtandao wa mtoa huduma, ikimpa mtumiaji uwezo wa kupiga simu, kutuma ujumbe, na kutumia data za intaneti.

Hapo zamani, tulianza laini kubwa za simu zilizojulikana kama Full-size SIM, ambazo baadaye zilipunguzwa hadi Mini-SIM, kisha Micro-SIM na hatimaye Nano-SIM ambazo ndizo zinazotumika sana kwa sasa.

Kila hatua ya mabadiliko haya ililenga kupunguza ukubwa wa kadi ya SIM ili kutoa nafasi zaidi ndani ya simu kwa vifaa vingine muhimu kama vile betri kubwa na vifaa vya mawasiliano.

SIM ni kifupi cha Subscriber Identity Module, ambayo ni kadi maalum inayotumika kuhifadhi taarifa za mtumiaji wa mtandao wa simu, Picha | Encriptados.

Hata hivyo, pamoja na kupungua kwa ukubwa wa SIM, hitaji la kubadilisha laini kwa mikono lilikuwa bado kikwazo. 

Hapo ndipo teknolojia ya eSIM ilipoibuka, ikiwa suluhisho la kidigitali linalomwezesha mtumiaji kubadili mtandao bila hitaji la kubadilisha kadi ya SIM kwa mikono.

eSIM ni nini?

eSIM, au “Embedded SIM,” ni kadi ya SIM ya kidigitali ambayo imejengewa moja kwa moja ndani ya simu au kifaa kingine cha mawasiliano. 

Tofauti na laini za kawaida zinazoweza kuondolewa na kubadilishwa, eSIM inafanya kazi kupitia programu maalum inayoruhusu mtumiaji kusajili na kubadili mitandao kwa urahisi bila kutumia kadi halisi. 

Teknolojia hii inaleta mapinduzi katika sekta ya mawasiliano kwa kuondoa hitaji la kubeba na kubadilisha laini za plastiki kila mara unapotaka kutumia mtandao tofauti.

eSIM, au “Embedded SIM,” ni kadi ya SIM ya kidigitali ambayo imejengewa moja kwa moja ndani ya simu au kifaa kingine cha mawasiliano. Picha | Paperjam.lu

Kwa Tanzania, huduma ya eSIM inapatikana kwa sasa kupitia mitandao ya Vodacom, Tigo, Airtel, na Halotel ambapo wateja wanaweza kuhamia eSIM kwa kutembelea maduka yao rasmi.

Faida za eSIM

Tofauti na watumiaji wa laini za simu za kawaida, watumiaji wa eSIM wanaweza kubadilisha mitandao kwa urahisi bila hitaji la kununua au kubadilisha kadi ya SIM. 

Kwa mfano, ukiwa na laini ya Vodacom lakini unataka kutumia Airtel, unaweza kufanya hivyo bila matatizo kama vile unavyo ingia na kutoka katika akaunti zako za mitandao ya kijamii.

Kutokana na kuwa eSIM haiondolewi kwenye simu kama laini za kawaida, inapunguza hatari ya kupoteza au kuibiwa laini ya simu yako. Hivyo humwezesha mtumiaji kuweza kutunza taarifa binafsi kwa uangalifu mkubwa. 

eSIM haiondolewi kwenye simu kama laini za kawaida, inapunguza hatari ya kupoteza au kuibiwa laini ya simu yako, Picha | Hero Image

Pia kwa kuwa eSIM haichukui nafasi kama SIM za kawaida, inatoa nafasi zaidi kwa vifaa vingine ndani ya simu, kama betri kubwa au teknolojia za hali ya juu.

eSim pia inafaa kwa wasafiri wa kimataifa kwa kuwa unaweza kununua huduma ya mtandao wa nchi husika bila kununua laini mpya.

Kwa mfano, mtumiaji wa Tigo Tanzania anapokuwa Dubai anaweza kutumia mtandao wa nchi hiyo bila hitaji la kubadilisha laini.

Changamoto za eSIM

Mbali na ubora au faida zinazotokana na eSim, teknolojia hii ina changamoto zake, kwa kuwa  si kila mtandao unatoa huduma ya eSIM ingawa kwa Tanzania mitandao ya simu kama Vodacom, Tigo, Airtel na Halotel imeshaanza kutoa huduma hii, ijapokuwa bado haijawa ya kawaida kwa watoa huduma wote nchini.

Pia sio kila simu inaweza kutumia eSIM, inahitaji simu ambazo zina uwezo wa kuunga mkono teknolojia hiyo, hivyo wamiliki wa simu za zamani hawana uwezo wa kufurahia teknolojia hii bila kubadili simu.

Sio kila simu inaweza kutumia eSIM, inahitaji simu ambazo zina uwezo wa kuunga mkono teknolojia hiyo, Picha | Dignited

Kwa kuwa kila kitu kipo kidigitali, hitilafu ya programu au tatizo la mtandao linaweza kufanya laini yako kushindwa kufanya kazi kwa muda fulani kwa kuwa teknolojia ya eSim inategemea zaidi huduma za mtandao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks