Jinsi ya kukabiliana na sonona kabla na baada ya kujifungua

February 7, 2025 12:46 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kukaa karibu na mume, wanafamilia baada ya kujifungua.
  • Wataalamu wa afya wanasema sonona huweza  kusababisha mama kujiua mwenyewe au kumuua mtoto.

Arusha. Kupata mtoto ni jambo la furaha kwa baadhi ya wazazi hususani waliopata mtoto kwa mara ya kwanza.

Shauku ya malezi na kuongeza mwanafamilia mpya huwagubika wapendanao hao kiasi cha kusahau kughulikia masuala mengine yanayowazunguka ikiwemo sonona.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), sonona ni hali ya kiakili inayoathiri hisia na uwezo wa mtu kufanya kazi za kila siku ikikadiriwa kuathiri watu zaidi ya milioni 280 duniani kote huku zaidi ya asilimia 50 wakiwa ni wanawake.

Pamoja na takwimu hizo WHO inabainisha kuwa asilimia 10 ya wanawake wajawazito duniani na asilimia 13 ya wale waliojifungua hukutana na tatizo hilo.

“Katika nchi zinazoendelea, hali hii ( sonona) ni ya juu zaidi kwa asilimia 15.6 wakati wa ujauzito na asilimia 19.8 baada ya kujifungua. Matatizo haya yanaweza kuwa makubwa akiasi cha kusababisha mama kujiua,” imesema WHO.

Evarista Jacob ni miongoni mwa wanawake waliokutana na tatizo la sonona lilioanzia wakati wa ujauzito na baadae kuendelea kumuathiri alipojifungua mtoto wake wa kwanza.

“Nilivyojigundua tu kuwa ni mjamzito hapo ndipo tatizo lilipoanzia, sikuwa na furaha nilikuwa nawaza kuwa huenda nimewahi sana kubeba ujauzito pia kila nikiwaza kuwa baada ya miezi tisa nitaitwa mama ndiyo nachanganyikiwa  kabisa,” anasema Evarista ambaye kwa sasa ni mama wa mtoto mmoja.

Evarista ameiambia Nukta habari kuwa hali hiyo ya msongo wa mawazo ilidumu katika miezi ya mwanzoni mwa ujauzito ambapo pia alisumbuliwa sana na homa za asubuhi ‘morning sickness’ zinazoambatana na kutapika, kichefu chefu na uchovu.

Hali hiyo ilirudi tena akiwa na siku moja tu baada ya kujifungua kwa upasuaji ikichangiwa zaidi na maumivu pamoja na kucheleweshwa kujifungua.

“Nilipata uchungu kwa masaa 12 nikijaribu kuzaa kwa njia ya kawaida mpaka madaktari walivyoona nimeishiwa nguvu na mtoto wangu tumboni amechoka ndipo nikapelekwa ‘theatre’ (chumba cha upasuaji).” amesema Evarista.

Changamoto hizo zilimfanya Evarista kupata msongo wa mawazo kwani alijiandaa kuzaa kawaida na hakutamani kuuguza kidonda kilichotokana na upasuaji.

Hivi sasa ni miezi minne tangu ajifungue lakini anakiri kutokuwa sawa huku hali ya msongo wa mawazo ikimsababishia tatizo la kusahau ambalo bado anakabiliana nalo.

Madaktari waeleza sababu

Nukta habari imezungumza na Dk Benjamin Kimaro, daktari bingwa wa masuala ya wanawake kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambaye anakiri kutokuwepo wa sababu rasmi za tatizo hilo licha ya kukutana na wenye hali hiyo kila siku.

“Ni kweli tatizo hili lipo na ninakutana na wagonjwa wa aina hiyo kila siku… ukweli ni kwamba hakuna sababu ya moja kwa moja inayochangia hali hii inaweza kuwa ni kutokujiandaa vyema au kutokuwa na maelewano mazuri na wenza wao…

….Kiufupi ni kwamba kila mwanamke anayekutana na hali hiiyo huwa ana sababu zake na huwa tunashirikiana na wanasaikolojia kuwasaidia,” amesema Dk Kimaro.

Kwa upande wake Patrick Motto mwanasaikolojia kutoka Shirika la Brac Tanzania anasema sababu nyingine inayioweza kuchangia sonona kipindi cha ujauzito  na baada ya kujifungua ni mabadiliko ya maumbile pamoja na kuongezeka kwa majukumu mapya.

“Unakuta mjamzito hakujiandaa na mabadiliko ya kimaumbie kama kunenepa sana au wengine wakisha jifungua tu majukumu maoya yanaongezeka ikiwemo ya malezi

… ile hali inakuwa inamchahanya mama na inampa wasiwasi ambao unasababisha msongo wa mawazo,” amesema Motto.

Kwa mujibu wake, ikiwa matatizo haya hayatatuliwa mapema mwanamke anaweza kupata matatizo ya afya aya akili ikiwemo kichaa cha mimba au wengine kutupa watoto 

“Utaona kuwa kuna watu wanatupa watoto hii yote inasababishwa na ‘postpartum depression’ lakini pia  kuna watu huugua uchizi au wasiwasi uliopitiliza na wengine ndoa kuvunjika,” ameeeleza Motto.

Naye Daktari Hussein Mugyabuso kutoka Hospitali ya Taifa Mnazi Mmoja ameeleza kuwa mara kadhaa sonona baada ya kujifungua huweza kusababisha mama kujiua yeye mwenyewe au kumdhuru mtoto.

“Ukiona hali kama hizo za sonona kwa mzazi ni vyema kukaa naye karibu na kumpokonya mtoto mpaka pale atakapokaa sawa kwa sababu wakati wowote ule anaweza kumdhuru au kujiua yeye mwenyewe,” amebainisha Dk Mugyabuso.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, kuongezeka kwa majukumu mapya na kubadilika kwa mwili ni miongoni mwa sababu za sonona baada ya kujifungua.Picha|American Councelling Association.

Jinsi ya kukabiliana na sosona

Dk Kimaro amesema kuwa ikiwa sonona itadumu kwa zaidi ya wiki mbili ni lazima mama aliyejifungua apate msaada wa kuonana na wataalamu wa saikolojia ili kuepusha madhara yanayoweza kujikeza.

“Hali ikiwa mbaya sana huwa tunawapa dawa kwa kushirikiana  na wenzetu wanasaikololojia ambao huwapa msaada zaidi iili kuwatoa katika hali hiyo,” amebainisha Dk Kimaro.

Aidha, Dk Mugyebuso ameshauri wanafamilia kuwa karibu na wanawake waliojifungua katika kipindi hicho ambacho wanakuwa hawapo sawa huku wakiendelea kujifunza kukabiliana na majukumu mapya.

Anasema kuwa kipindi hicho sio wakati wa kumlaumu mama kwa mabadiliko yoyote ya mwili wake au kwa njia ya uzazi ambayo ameichagua na ikiwa ni mtoto wake wa kwanza basi mume pamoja na wanafamilia wengine wanatakiwa kuwa naye karibu zaidi.

Msaikolojia Patrick Motto naye amewashauri wajawazito kuhudhuria kliniki katika miezi yote ya ujauzito na kuweka wazi hali yoyote anayoipitia ikiwemo msongo wa mawazo ili aweze kusaidiwa.

“Kwa kuwa hakuna sababu maalum ya tatizo hili hivyo nawashauri wajawazito kuhudhuria kliniki kwa wakati na kuzungumza na wanasaikolojia au madaktari mara wanapohisi dalili za msongo wa mawazo.” ameeelza Motto.

Pia amewashauri wanaume kutowakimbia wanawake zao katika kipindi hiki na kuanzisha mahusiano na wanawake wengine nje, jambo hili huchochea msongo wa mawazo kwa mama aliyejifungua na kuathiri malezi ya mtoto.

“Mwili wa mwanamke huzalisha homoni za ‘octoson’ ambazo zinazalisha bondi inazoleta ukaribu kawa mama na mtoto hii hali huwafanya wanaume wengi kuanzisha mahusiano nje kwa kuwa wanaona mwanamke anamjali sana mtoto…

Niwashauri wanaume kipindi cha ujauzito na wakati wa kujifungua ndiyo kipindi cha kuwa karibu na mkeo kuliko wakati mwingine wowote ili kuweza kuepuka madhara haya ambayo tunayazungumzia,” ameongeza Motto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks