WHO yamteua Dk Chikwe Ihekweazu kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika

February 5, 2025 4:31 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Uteuzi huo unakuja baada ya kifo cha Dk Faustine Ndugulile, huku Tanzania ikiwa tayari kushiriki tena kwenye mashindano ya uongozi wa WHO.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, amemtangaza Dk Chikwe Ihekweazu kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 5, 2025 na WHO kupitia ukurasa wake wa X imebainisha kuwa uteuzi huu unafanyika wakati Dk Matshidiso Moeti anapomaliza muda wake wa kuhudumu kama Mkurugenzi wa WHO katika kanda hiyo.

Dk Ihekweazu, ambaye hapo awali alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Nigeria (NCDC), ana uzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika sekta ya afya ya umma na udhibiti wa magonjwa.

Dk Chikwe Ihekweazu Kaimu Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika. Picha/ WHO African Region.

Kabla ya uteuzi huu, alikuwa akihudumu kama Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa WHO, akiongoza Kituo cha Kujitayarisha kwa Dharura za Afya (WHO Hub for Pandemic and Epidemic Intelligence) huko Berlin, Ujerumani.

Akiwa mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza, Dk Ihekweazu ameongoza na kushiriki katika juhudi za kimataifa za kukabiliana na magonjwa kwa miaka mingi. 

Pia, amefanya kazi katika taasisi mbalimbali za afya duniani, ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Kitaifa ya Magonjwa ya Kuambukiza ya Afrika Kusini (NICD), Shirika la Ulinzi wa Afya la Uingereza (HPA) na Taasisi ya Robert Koch ya Ujerumani (RKI). 

Uteuzi huu unakuja katika kipindi ambacho WHO inaendelea na juhudi za kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika ili kukabiliana na changamoto za magonjwa. 

Hata hivyo, uteuzi huu pia unahusiana na mabadiliko yaliyotokea baada ya kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi mteule wa WHO Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile, aliyefariki dunia Novemba 27, 2024, nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.

Baada ya kifo hicho, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wakati wa hafla ya kuaga mwili wa Dk Ndugulile, alibainisha kuwa Tanzania itamuandaa mgombea mwingine mwenye sifa kushindania nafasi ya ukuu wa WHO Kanda ya Afrika. 

Rais Samia pia alisisitiza kuwa nchi haitakata tamaa katika kuhakikisha kuwa inapata mwakilishi mwingine mwenye sifa za kutosha kuwania nafasi hiyo.

“Wanadamu tunapanga yetu, lakini Mungu anatupangia. Dk Ndugulile ameiweka nchi pazuri lakini Mungu amechukua kilicho chake. Tutaingia tena kwenye mashindano, tutatafuta Mtanzania mwenye sifa anayeweza kushindana na ulimwengu, tutaweka mtu mwenye sifa ileile kutuwakilisha,” alisema Rais Samia Desemba 2, 2024.

Uteuzi wa Dk Ihekweazu unaleta matumaini mapya kwa sekta ya afya barani Afrika, huku jitihada zikiendelea kufanywa ili kuimarisha afya ya umma na kuhakikisha Afrika inaendelea kuwa na mifumo bora ya kukabiliana na changamoto za magonjwa.

Sanjari na hayo WHO pia wamebainisha kuwa uteuzi wa mgombea mwingine atakayekuwa Mkurugenzi Mkuu wa WHO Kanda ya Afrika unatarajiwa kufanyika Mei.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks