Serikali kufanya sensa ya uzalishaji viwandani Machi 2025

February 4, 2025 3:32 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Matokeo ya sensa hiyo yatatumika kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) na Dira ya Afrika Mashariki 2050.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imetangaza kufanyika kwa Sensa ya Uzalishaji Viwandani kwa Mwaka wa Rejea 2023 mwezi Machi 2025. 

Sensa hiyo, ambayo ni ya kwanza kufanyika kwa pamoja Tanzania bara na Zanzibar tangu mwaka 1964, inatarajiwa kutoa taarifa za kina za kitakwimu zitakazosaidia kuboresha sera na mipango ya maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.

Awali sensa ilikuwa ikifanyika kwa awamu tofauti ambapo Tanzania Bara ilifanyika mwaka 1963, 1978, 1989 na 2013, na kwa upande wa Zanzibar, zilifanyika mwaka 1989, 2002, 2008 na 2012.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Selemani Jafo leo Februari leo 4, 2025, sensa ya mwisho ya viwanda ilifanyika mwaka 2013 ikibainisha uwepo wa viwanda 49,243 nchini. 

“Viwanda hivyo viligawanywa katika makundi manne ambayo ni viwanda vidogo sana 41,919, viwanda vidogo (6,907), viwanda vya kati (170), na viwanda vikubwa (247),’’ imefafanua taarifa hiyo.

Taarifa imeongeza kuwa, Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ilionyesha kuwa idadi ya viwanda imeongezeka hadi kufikia 69,106, ikiwa ni pamoja na viwanda vidogo sana (53,464), viwanda vidogo (13,367), viwanda vya kati (1,614), na viwanda vikubwa (661).

Waziri Jafo ameongeza kuwa mwaka 2023 sekta ya viwanda ilisajili miradi 208 yenye thamani ya dola za Marekani 1.68 milioni sawa na Sh4.30 trilioni za Kitanzania na kutengeneza fursa za ajira 26,563. 

Hata hivyo, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) lilitoa mafunzo kwa wajasiriamali 22,139 kwenye mada mbalimbali kama vile usindikaji wa mafuta, utengenezaji wa bidhaa za ngozi, na mbinu za uzalishaji.

Waziri Jafo pia amebainisha kuwa, Sensa ya Uzalishaji Viwandani ya Mwaka wa Rejea 2023 inalenga kukusanya taarifa za kitakwimu zitakazosaidia Serikali na wadau kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya kuboresha sekta ya viwanda na uchumi wa kitaifa kwa ujumla. 

Taswira ya Kiwanda cha kuzalisha saruji cha Twiga (Twiga Cement) kilichopo Tegeta jijini Dar es Salaam. Picha/Ministry of Foreign Affairs and East African Cooperation.

Matokeo ya sensa hiyo yatatumika pia kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III), Dira ya Afrika Mashariki 2050, Agenda ya Maendeleo ya Afrika 2063, na Malengo Endelevu ya Dunia 2030 (SDGs), hasa kuhusu upatikanaji wa maji safi, nishati, na maendeleo ya viwanda.

Utengenezaji wa bidhaa, uchimbaji wa madini, uzalishaji wa umeme na gesi, na usambazaji wa maji safi ni miongoni mwa shughuli za kiuchumi zitakozofanyika . 

“Taarifa zitakusanywa kutoka kwa viwanda vyote vilivyogawanywa katika makundi mawili, viwanda vyenye wafanyakazi kuanzia kumi na zaidi, na viwanda vyenye wafanyakazi kuanzia mmoja hadi tisa,’’ imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, ukusanyaji wa taarifa utafanyika kwa kutumia mfumo wa kielektroniki, sawa na ulivyotumika wakati wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022. 

Wakati huo huo, wadadisi watatumia vifaa vya kielektroniki kukusanya taarifa kwa ufanisi na usahihi.

Wito kwa wadau wa sekta ya viwanda

Hata hivyo, Waziri Jafo amewataka wamiliki wa viwanda na wadau wote wa sekta hiyo kushirikiana na Serikali ili kufanikisha zoezi hilo.

Sensa ya Uzalishaji Viwandani kwa Mwaka wa Rejea 2023 inafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu sura ya 351. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, taarifa zote zinazokusanywa wakati wa sensa na tafiti zitakuwa ni siri na zinatumika kwa madhumuni ya kitakwimu pekee,’’ amesema Waziri Jafo. 

Aidha, onyo kali limetolewa kwa wenye viwanda iwapo watabainika kukataa kutoa taarifa sahihi za viwanda vyao kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria. 

Waziri Jafo ameonesha msisitizo kwa kuwataka wadau mbalimbali kushirikiana ili kufanikisha zoezi hili ikiwa ni pamoja na wa wadau wa sekta ya viwanda wakiwemo wamiliki, menejimenti na taasisi zinazosimamia na zinazounganisha wadau hao katika ngazi zote za utawala.

Pia, wadau wote katika sekta ya viwanda nchini wametakiwa kuhakikisha wanashirikiana na Serikali kufanikisha utekelezaji wa sensa hiyo na kutoa ushirikiano kwa kuelimisha na kuhamasishana kushiriki katika sensa hii na kutoa taarifa sahihi kwa mujibu wa maswali yatakayoulizwa. 

Ikumbukwe kuwa, suala la takwimu ni miongoni mwa mambo ya muungano (namba 20 kwenye orodha ya mambo ya muungano) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks