Jafo aunda kamati kushughulikia ongezeko wafanyabiashara wa kigeni Kariakoo

February 3, 2025 1:12 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Kamati hiyo itaongozwa na Profesa Edda Luoga Mkuu wa Chuo cha Biashara (CBE).
  • wajumbe walioteuliwa ni kutoka taasisi  za umma, binafsi na wawakilishi wawili wa wafanyabiashara Kariakoo.

Arusha. Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Selemani Jafo ameunda kamati ya wajumbe 16 watakaoshughulikia changamoto ya kuongezeka kwa wafanyabiashara wa kigeni katika soko la Kimataifa Kariakoo.

Waziri Jafo ameunda Kamati hiyo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyeiagiza wizara hiyo kuhakikisha raia wa kigeni hawajihusishi na biashara zinazopaswa kufanywa na wazawa, kufuatilia utoaji wa leseni za biashara kwa wazawa na wageni ikiwa ni pamoja na kusajili wafanyabiashara na kuwa na kanzidata yao. 

Kamati hiyo inayoundwa na wajumbe 16 itafanya kazi kwa siku 30 na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kutatua changamoto hiyo iliyokuwa ikilalalmikiwa kwa muda mrefu na wafanyabiashara wa Kariakoo.

Taarifa ya Dk Jafo iliyotolewa Februari 2, 2025 inabainisha kuwa wajumbe walioteuliwa ni kitoka taasisi  za umma, binafsi na wawakilishi wawili wa wafanyabiashara ikiongozwa Profesa Edda Luoga Mkuu wa Chuo cha Biashara (CBE) ambaye atakuwa mwenyekiti.

“Wajumbe wa Kamati hiyo iliyoundwa kutekeleza maelekezo hayo ni kama ifuatavyo Prof  Edda  Luoga, Mkuu wa Chuo cha Biashara (CBE), Sempheo Nyari, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara, Wizara ya Viwanda na Biashara (Katibu),” Iimesema taarifa ya Jafo.

Wajumbe wengine walioteuliwa ni pamoja na Francis Maro, Naibu Kamishna wa Polisi, Kigongo Shile, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Latifa Khamis Mohamed, Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) na  Gilead John Teri, Mkurugenzi Mkuu, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Wengine ni Godfrey Nyaisa, Mtendaji Mkuu, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), William Erio, Mkurugenzi Mkuu, Tume ya Ushindani (FCC), Ted Frank Kamishna Huduma za Ufundi, Idara ya Kodi za Ndani, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Timu hiyo pia imewahusisha wajumbe wengine akiwemo Beda Masoud, Katibu Tawala Msaidizi – Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mkoa wa Dar es Salaam, Lilian Denis Francis, Kamishna Msaidizi-Vibali vya Kazi, OWM – Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Elihuruma Mabelya, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam na Raphael Maganga, Afisa Mtendaji Mkuu, Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Aidha, kamati hiyo pia imewahusisha viongozi wa wafanyabiashara akiwemo Hamisi Livembe, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania,Severin Mushi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo na Leonce Bilauri, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Itifaki, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Pamoja na uteuzi wa kamati hiyo taarifa ya Jaffo inafafanya kuwa wajumbe wa Kamati hiyo wataongezwa kwa kadri ya mahitaji yatakayobainika. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks