Faida za kula matunda makavu katika mlo wa kila siku
- Ni pamoja na kusaidia mmeng’enyo wa chakula na afya ya moyo.
- Kupunguza madhara ya seli mwilini kulingana na uwepo vioksidishaji vilivyomo kwenye matunda.
Ulaji wa matunda ni jambo linalosisitizwa na wataalamu wa afya kutokana na umuhimu wake katika kuimarisha afya ya binadamu.
Hata hivyo, watu wengi hupendelea zaidi matunda mabichi huku wakipuuzia matunda makavu au kuyatumia katika mapishi mbalimbali jambo linaloweza kupunguza virutubisho muhimu vilivyopo katika matunda hayo.
Kwa mujibu wa Afisa Lishe kutoka Hospitali ya Kondoa, Irine Kweka, iliyopo jijini Dodoma amebainisha kuwa faida za ulaji matunda makavu hazina utofauti mkubwa na zile zinazopatikana kwenye matunda ya kawaida.
“Matunda makavu yenyewe hayana maji maji ile ‘moisture contents’ (unyevu nyevu) imetoka, hivyo yana ’fibres’( nyuzi nyuzi) na vitamini kwa wingi,” ameeleza Kweka.
Matunda makavu na faida zake
Kwa mujibu wa tovuti ya Healthline, matunda makavu hupatikana baada ya maji kuondolewa kupitia mchakato wa kukaushwa, hivyo kuwa na msongamano mkubwa wa nishati.
Matunda maarufu zaidi katika kundi hili ni zabibu kavu, tende, tini na aprikoti.
Wakati huo tovuti ya Good Food inabainisha kuwa gramu 30 za matunda makavu huchukuliwa kama sehemu mojawapo ya ulaji wa matunda na mboga tano kwa siku.
Kwa mfano, gramu 30 za zabibu kavu hutoa kalori 82, protini 0.6g, wanga 20.8g, sukari 20.8g, potasiamu 306mg na nyuzi nyuzi 0.8g.
Chanzo kikubwa cha virutubisho
Kweka amesema kuwa matunda yaliyokaushwa ni chanzo kizuri cha virutubisho, hasa nyuzinyuzi ambazo ni sehemu muhimu ya lishe inayosaidia mmeng’enyo wa chakula na inaweza pia kusaidia afya ya moyo na udhibiti wa kiwango cha sukari mwilini.
Matunda kama zabibu kavu na tini (figs) ni maarufu kwa kusaidia utumbo kufanya kazi vizuri.
Sanjari na hayo pia Kweka amebainisha kuwa zabibu kavu huwa na vitamini C ambazo husaidia katika kuimarisha kinga mwili.
Chanzo cha hemoglobini
Faida moja kubwa ya matunda yaliyokaushwa ni kwamba yana madini ya chuma kwa wingi, ambayo husaidia katika utengenezaji wa hemoglobini.
Kwa sababu hiyo, matunda haya yanaweza kusaidia kupambana na upungufu wa damu (anemia).
Pia yana asidi ya foliki, ambayo huchangia katika uzalishaji wa chembe nyekundu za damu, na vitamini C inayosaidia mwili kunyonya madini ya chuma kwa urahisi.
Ikiwa unahitaji kuongeza kiwango cha chuma mwilini, kula matunda yaliyokaushwa kunaweza kusaidia.
Husaidia kuzuia saratani na kisukari
Vioksidishaji vilivyomo kwenye matunda makavu kama zabibu, ‘blueberries’ na ‘cranberries’ vina uwezo wa kupunguza madhara ya seli mwilini, hivyo kusaidia kuzuia magonjwa sugu kama kisukari na saratani.
Kwa mujibu wa tovuti ya Metropolis, utafiti unaonyesha kuwa matunda yaliyokaushwa yanaweza kusaidia kupunguza hatari ya saratani.
Kwa mfano, ulaji wa tunda la aprikoti zilizokaushwa mara kwa mara unaweza kupunguza hatari ya kupata saratani ya ovari na kuongeza ulinzi dhidi ya saratani ya utumbo mpana.
Pia, aprikoti zilizokaushwa zina beta-carotene, ambayo mwili hubadilisha kuwa vitamini A.
Kiwango chake cha juu cha nyuzinyuzi husaidia kuweka mfumo wa usagaji chakula katika hali nzuri, huku antioxidants zikipunguza uvimbe mwilini.
Kuimarisha afya ya mifupa
Matunda yaliyokaushwa ni chanzo bora cha virutubisho vinavyosaidia afya ya mifupa. Kwa mfano, aprikoti zilizokaushwa zina kiasi kikubwa cha kalsiamu, ambayo ni muhimu kwa mifupa imara.
Plamu kavu pia zina madini ya magnesiamu na potasiamu, ambayo husaidia kudumisha msongamano wa mifupa.
Zaidi ya hayo, matunda haya yanaweza kusaidia kupunguza uvimbe na kuzuia uharibifu wa seli.
Utafiti uliofanya na jarida la Health Journal of Medicine unaonyesha kuwa plamu kavu zinaweza kusaidia afya ya mifupa, ikiwa ni pamoja na kupunguza kasi ya upotevu wa mifupa unaotokea katika umri wa kati hasa kwa wanawake waliokoma hedhi.
Kiwango cha juu cha virutubisho vinavyosaidia mifupa, kama vile vitamini K na boroni, katika matunda yaliyokaushwa kama prune, huenda kikawa sababu ya faida hizi.
Kwa hivyo, kula kiasi kidogo cha matunda yaliyokaushwa kila siku kunaweza kusaidia kuimarisha mifupa yako.
Husaidia kupunguza uzito
Matunda yaliyokaushwa yanaweza kusaidia kupunguza uzito, tofauti na matunda mabichi ambayo mara nyingi huwa na kiwango kikubwa cha sukari, matunda yaliyokaushwa yana sukari kidogo na kalori chache zaidi.
Pia yana nyuzi nyuzi nyingi, ambazo husaidia kukufanya ujisikie kushiba kwa muda mrefu.
Hii inamaanisha kuwa kula matunda yaliyokaushwa kunaweza kusaidia kudhibiti hamu ya kula na kupunguza ulaji wa vyakula visivyo na virutubisho.
Husaidia katika uchungu wa kujifungua
Kwa upande wa Jarida la Journal of Midwives and Reproductive Health, limebainisha kuwa kula matunda yaliyokaushwa, hasa tende, katika wiki za mwisho za ujauzito kunaweza kusaidia kulainisha mlango wa kizazi.
Hii ni kutokana na utafiti wa majaribio uliofanywa Februari 1, 2007 na Januari 31, 2008 katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jordan ambao ulibainisha kuwa matumizi ya tende kwa wanawake wajawazito husaidia kupunguza makali ya uchungu.
Ni muhimu kuchagua matunda makavu yasiyo na sukari au kemikali zilizoongezwa ili kupata manufaa bora kiafya.