Lissu ashinda uenyekiti Chadema – Mbowe
- Hadi sasa matokeo rasmi ya uchaguzi huo hayajatangazwa ila Mbowe ameshakubali kushindwa.
Dar es Salaam. Mwanasiasa machachari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu amechaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho kuwa mwenyekiti akimbwaga kiongozi wa muda mrefu, Freeman Mbowe.
Lissu, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Chadema, alikuwa akichuana vikali na Mbowe ambaye amekiongoza chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka 20.
Mbowe ameeleza katika ukurasa wake rasmu wa mtandao wa X kuwa amepokea kwa mikono miwili maamuzi ya uchaguzi wa mkutano mkuu wa chama chao uliohitimisha leo asubuhi.
“Nampongeza Mheshimiwa Tundu Lissu na wenzake kwa kuaminiwa kutwikwa jukumu la uongozi wa chama. Nawatakia kila la kheri katika kukipeleka mbele chama chetu,” amesema Mbowe.
Hadi sasa bado wasimamizi wa uchaguzi huo bado hawajatoa matokeo rasmi ya uchaguzi huo licha ya wagombea kueleza matokeo ya awali.