Rais Samia athibitisha uwepo wa Marburg Tanzania

January 20, 2025 5:59 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mtu mmoja abainika kuwa na virusi vya ugonjwa huo usiokuwa na tiba wala kinga mkoani Kagera.

Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amesema mtu mmoja ameathirika na virusi vya ugonjwa wa Marburg ikiwa ni siku tano tangu Shirika la Afya Duniani (WHO) kuripoti juu ya uwepo wa vifo nane kati ya wahisiwa tisa wa maradhi hayo mkoani Kagera. 

Kugundulika kwa mtu huyo, kunaifanya Tanzania iliripoti uwepo wa maradhi hayo yasiyokuwa na chanjo wala tiba kwa mara ya pili ndani ya miaka miwili katika mkoa huo wa Kaskazini magharibi mwa nchi. 

Mara ya kwanza ugonjwa huo uliripotiwa Machi, 2023 na kudumu kwa miezi miwili ukisababisha vifo vya watu sita kati ya tisa waliogundulika kuwa na virusi hivyo.

Katika mkutano na wanahabari Ikulu jijini Dodoma pamoja na Mkurugenzi wa WHO Dk Tedros Ghebreyesus leo Januari 20, 2025, Rais Samia amesema mara baada ya kupata taarifa ya uwepo wa virusi vya Marburg Serikali ilichukua hatua za haraka ikiwemo kufanya uchunguzi wa washukiwa na ufuatiliaji wa wahisiwa kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa. 

“Vipimo vya maabara vilivyofanyika katika maabara ya Kabaile huko Kagera, na baadaye kuthibitishwa Dar es Salaam, vilibaini mgonjwa mmoja aliyeambukizwa virusi vya Marburg. Kwa bahati nzuri, wagonjwa wengine waliodhaniwa walipimwa na kugundulika kuwa na magonjwa mengine,” amesema Rais Samia. 

Katikati mwa wiki iliyopita, WHO iliripoti uwepo wa wahisiwa tisa wa Marburg huku nane wakifariki dunia. Hata hivyo, Wizara ya Afya ilikanusha uwepo wa ugonjwa huo ikieleza  kuwa sampuli zilizochukuliwa kwa wahisiwa hazikuthibitisha uwepo wa virusi hivyo. 

“Chanzo cha vifo vilivyoripotiwa hapo awali kwenye eneo husika bado hakijathibitishwa na jitihada zinaendelea kubaini chanzo halisi,” amesema Rais Samia. 

Hadi kufikia leo,  Rais Samia ameeleza kuwa kuna jumla ya wahisiwa 25 ambao baada ya kupimwa hawakukutwa na virusi na kwamba wanaendelea kuwafuatilia kubaini afya zao. 

“Tunapenda kuwahakikishia wote kwamba hatua zilizochukuliwa wakati wa mlipuko wa kwanza wa 2023, ambazo zilijumuisha kutengwa kwa haraka, matibabu ya visa, ufuatiliaji wa mawasiliano, na ushirikishwaji wa jamii…tuna imani kuwa tutashinda changamoto hii tena,” amesema Rais Samia.

Kwa mujibu wa WHO, dalili za ugonjwa huo ni pamoja na maumivu ya kichwa, mgongo, homa kali, kuhara, kutokwa na damu (kutapika kwa damu), malaise (udhaifu wa mwili) na katika hatua ya baadae mgonjwa hutokwa na damu sehemu zenye matundu ikiwemo puani.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Tedros Ghebreyesus, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.Picha|Ikulu Mawasiliano.

Zaidi ya bilioni 7 kupambana na Marburg Tanzania

Dk Tedros amewaambia wanahabari kuwa WHO imetoa Dola za Marekani milioni 3 (sawa na Sh 7.4 bilioni) zitakazosaidia kupambana na ugonjwa huo.

Bosi huyo wa WHO amesema Tanzania ina uzoefu wa kukabiliana na Marburg baada ya kuutokomeza ugonjwa huo takriban miaka miwili iliyopita. 

Dk Tedrois amebainisha kuwa mpaka sasa hakuna tiba dhidi ya ugonjwa huo na kuitaka Serikali ya Tanzania kuwekeza zaidi katika kuudhibiti kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo zile zilizotumika mwaka 2023.

“Kwa sababu ya kiwango kidogo cha vihatarishi vya ugonjwa huu duniani na uimara wa Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na maradhi haya, WHO haishauri kuwekwa vikwazo vyovyote vya kibiashara wala safari kuingia nchini,” amesema huku akieleza kuwa “Tanzania ipo wazi kibiashara”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks