Rukwa, Morogoro wasalia vinara wa ulaghai mtandaoni ukipungua kwa asilimia 19
- Ndio mikoa inayoongoza kwa kuwa na zaidi ya theluthi moja ya matukio yote ya ulaghai nchini.
- Jumla ya matukio ya ulaghai 12,896 yaripotiwa.
Arusha. Licha ya kupungua kwa ulaghai mtandaoni kwa asilimia 19 nchini mikoa ya Rukwa na Morogoro imeendelea kuwa vinara wa kuripoti matukio hayo ndani ya kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Ulaghai huo unahusisha wizi wa fedha katika akaunti za mitandao ya simu au benki uliofanyika katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka 2024.
Takwimu za mawasiliano za robo ya mwaka unaoishia Disemba 2024 zinazotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinabainisha kuwa, Tanzania ilirekodi majaribio 12,896 yaliyopungua kutoka matukio 16,069 yaliyoripotiwa katika robo ya mwaka inayoishia Septemba 2025.
Wakati matukio hayo yanapungua nchini Mikoa ya Rukwa na Morogoro ndiyo inayoongoza, ikiwa na zaidi ya theluthi moja ya majaribio yote ya ulaghai nchini
Mkoa wa Rukwa umeripoti matukio ya ulaghai 5.305 yaliyoufanya kuwa kinara kwa matukio hayo ndani ya miezi mitatu iliyopita yakipungua kiduchu kutoka matukio 5,571 yaliyoripotiwa katika robo ya mwaka iliyoishia Septemba 2024.
Zaidi ya nusu ya matukio hayo sawa na matukio 3,795 yaliripotiwa katika Wilaya ya Sumbawanga Mjini ikifuatiwa na matukio katika Wilaya ya Sumbawanga vijijini.
Aidha, Mkoa wa Morogoro umeripoti matukio 4,278 ambapo zaidi ya asilimia 90 yameripotiwa katika Wilaya ya Kilombero.
Mikoa mingine iliyoongoza kwa matukio hayo ni Mbeya ulioripoti matukio 930, Dar es Salaam 762 na mkoa wa Katavi matukio 281.
Kwa upande wa mikoa Simiyu, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, kusini Pemba na Kaskazini Pemba ndiyo imeripoti idadi ndogo zaidi ya matukio hayo.
Jitihada mbalimbali ziilizofanywa na Serikali ikiwemo kuwachukulia hatua wahusika zimechangia kupunguza ulaghai mtandaoni.Picha|Lucy Samson.
Artel kinara wa ulaghai
Takwimu za TCRA zinabainisha kuwa mtandao wa Artel umeripoti jumla ya matukio 5,187 ikiwa ndiyo mtandao wenye idadi kubwa zaidi ya matukio hayo.
Matukio hayo katika mtandao wa Airtel yameongezeka kwa asilimia 52 kulinganisha na idadi ya matukio yaloyoripotiwa katika robo ya mwaka inayoishia Septemba 2024.
Mtandao wa Vodacom umeshika nafasi ya pili kwa kuripoti jumla ya matukio 2,902 yakipungua kwa asilimia tisa kutoka matukio 3,175 yaliyoripotiwa mwezi Septemba 2024.
Mitandao mingine ni TTCL ulioripoti matukio 2,391 pamoja na mtandao wa Yas ulioripoti matukio1,663.