Ukweli kuhusu nanasi kutoa mimba 

January 16, 2025 3:11 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataalamu wa afya wasema hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya ulaji wa nanasi na kuharibika kwa mimba.
  • Nanasi lina faida nyingi kiafya ikiwemo kuimarisha kinga ya mtoto aliyetumboni.

Arusha. Ni kawaida kwa wajawazito kushauriwa kula mlo kamili unaohusisha vyakula kutoka makundi yote ikiwemo mboga mboga na matunda.

Kundi hilo la chakula husaidia kuimarisha kingamwili za mama huku yakihakikisha upatikanaji wa virutubisho muhimu kwa mtoto aliyetumboni ikiwemo vitamini na madini chuma.

Licha ya umuhimu wa kundi la matunda na mboga kwa mjamzito, kumekuwa na baadhi ya taarifa zinazosambaa mitaani na katika mitandao ya kijamii zikiwatahadharisha wajawazito kutumia nanasi kwa kuwa linasababisha mimba kutoka.

Baadhi ya wasambazaji wa taarifa hiyo hususani katika mtandao wa Tiktok wanadai kuwa tunda la nanasi pamoja na matunda mengine kama zabibu hayafai kutumiwa kwa mjamzito hususani katika miezi mitatu ya mwanzo.

Moja kati ya video katika mtandao huo iliyopata watazamaji zaidi ya 1,300 inadai mjamzito akitumia tunda hilo kizazi chake kinaweza kupata moto na kufunguka hivyo kufanya mimba kutoka.

Nanasi lina wingi wa kemikali za asili ikiwemo  beta-carotene ambayo hubadilishwa na kuwa vitamin A na kuimarisha kingamwili.Picha| Modern Nona.

Ukweli ni upi?

Nukta habari imezungumza na wataalamu wa afya akiwemo Dk Benjamin Kimaro, daktari bngwa wa masuala ya wanawake kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili aliyebainisha kutokuwepo kwa tafiti rasmi zinazothibitisha suala hilo.

“Hizo ni taarifa za uvumi tu kama zilivyo taarifa nyingine, hakuna utafiti rasmi uliofanyika kuthibitisha kuwa nanasi lina uwezo wa kutoa mimba katika kipindi hicho ambacho kinatajwa,” amesema Dk Kimaro.

Aidha, amebainisha kuwa tunda hilo pekee halina uwezo wa kutoa mimba labda mjamzito awe ana changamoto nyingine za kiafya zinazohusiana na ulaji wa tunda hilo.

Naye Malimi Kitunda, mtaalamu wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) anasema matunda yenye rangi ya njano ikiwemo nanasi yana wingi wa kemikali za asili ikiwemo  beta-carotene ambayo Ina faida nyingi katika mwili wa binadamu pamoja na mama mjamzito.

Kemikali hiyo ikiingia mwilini hubadilishwa na kuwa vitamin A ambayo hufanya kazi mbalimbali ikiwemo kuimarisha afya ya ngozi,

“Kazi za vitamin A mwilini ni pamoja na kusaidia kuimarisha afya ya ngozi na kujifanya isizeke mapema, kusaidia macho kuona vizuri, kusaidia kuimalisha kinga ya mwili kupambana na magonjwa mbalimbali vile vile kusaidia ukuaji mzuri wa mimba na maendeleo ya mtoto aliye tumboni,” amesema Malimi.

Nini husababisha mimba kutoka

Kwa mujibu wa tovuti ya afya ya Tanzmend, mimba huharibika kutokana na kutokuwepo kwa uwiano wa vichocheo (hormonal inbalance) hasa upungufu wa kichocheo aina ya “progesterone” ambacho ni muhimu sana katika ukuaji wa mimba.

Sababu zingine ni pamoja na uvimbe kwenye kizazi, kulegea kwa shingo ya kizazi, mjamzito kuwa na kinga ya mwili dhaifu, kufanya kazi ngumu na kwa muda mrefu, kupigwa kwa mjamzito kwenye tumbo, utapiamlo na uzito uliopitiliza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks