Serikali: Sampuli hazijathibitisha uwepo wa Marburg Tanzania

January 16, 2025 10:27 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali yasema imeimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa nchini. 

Arusha. Serikali ya Tanzania imesema sampuli zilizochukuliwa kwa wahisiwa hazijathibitisha uwepo wa virusi vya Marburg katika mkoa wa Kagera, tofauti na taarifa zilizoripotiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na vyombo vya habari vya kimataifa kuwa watu nane wamefariki kwa ugonjwa huo.

Taarifa ya Waziri wa Afya, Jenista Mhagama iliyotolewa Januari 15, 2025 ikiwa ni saa chache baada ya WHO kuthibitisha uwepo wa ugonjwa huo inasema sampuli za wahisiswa hazikukutwa na maambukizi hayo.

“Mpaka leo tarehe 15 Januari 2025, majibu ya uchunguzi wa kimaabara kutoka kwa wahisiwa wote waliochukuliwa sampuli hizo hayajathibitisha uwepo wa virusi vya Marburg,” imesema taarifa ya Mhagama.

Hata hivyo, taarifa hiyo inakinzana na taarifa ya  WHO iliyotolewa Januari 14 mwaka huu ikibainisha kupokea taarifa za kuaminika juu ya uwepo wa ugonjwa huo Januari 10 mwaka huu.

“Kufikia tarehe 11 Januari 2025, jumla ya visa tisa vinavyoshukiwa vimeripotiwa nchini Tanzania, vikiwemo vifo vinane (kiwango cha vifo [CFR] cha 89%) katika wilaya za Biharamulo na Muleba, mkoa wa Kagera…

…Sampuli kutoka kwa wagonjwa wawili zimekusanywa na kufanyiwa uchunguzi katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Umma, huku matokeo yakisubiri uthibitisho rasmi. Watu waliokutana na wagonjwa hao, wakiwemo wahudumu wa afya, wametambuliwa na wako chini ya ufuatiliaji katika maeneo husika,”  imesema taarifa hiyo iliyochapishwa katika tovuti rasmi ya WHO.

WHO imesema dalili zilizoripotiwa ni zile zinazofanana za maumivu ya kichwa, homa kali, maumivu ya mgongo, kuhara, kutokwa na damu (kutapika kwa damu), malaise (udhaifu wa mwili) na katika hatua ya baadaye ya ugonjwa, kutokwa na damu kwa nje (kutokwa na damu kwenye matundu).

Ikiwa ugonjwa huo ukithibitishwa, itakuwa mara ya pili kwa ugonjwa huo kutokea mkoani Kagera baada ya kuripotiwa kutokea Machi, 2023 na kudumu kwa miezi miwili huku ukisababisha vifo vya watu sita.

Aidha, Wizara ya Afya imewahakikishia wananchi pamoja na jumuiya ya kimataifa kuwa imeimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa na kwamba itaendelea kutoa taarifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks