Fahamu namba za magari Tanzania na maana zake
- Ni pamoja na magari ya majeshi, wanadiplomasia na viongozi wa Bunge.
- Taratibu za utoaji namba hizo hutegemea sheria au miongozo ya namba husika.
Dar es Salaam. Namba za usajili za magari nchini Tanzania hubeba maana maalum kulingana na herufi na rangi ya vibao vyake. Hii inajumuisha magari ya viongozi, mashirika mbalimbali, na taasisi za serikali.
Pengine umejiuliza maana ya tofauti hizi na lengo lake. Je, unajua rangi ya kibao cha gari au herufi zilizo kwenye namba za usajili zinaashiria nini?
Ondoa shaka, makala hii ya inakufafanulia kwa undani aina tofauti za vibao vya usajili wa magari nchini Tanzania, herufi na rangi zinazotumika, pamoja na umuhimu wake.
Kibao chenye rangi ya njano
Hii ni aina ya kibao maarufu kinachoashiria kuwa gari limesajiliwa kwa matumizi binafsi (Private Use). Magari haya hayaruhusiwi kutumika kwa shughuli za kibiashara.
Pia, vibao vya aina hii vinaweza kuwa na majina ya watu au majina maalum, maarufu kama vibao vya “Customized”. Hii ni huduma inayolipiwa kwa mamlaka husika, na mara nyingi hutumiwa na wasanii na watu mashuhuri.
Kibao chenye rangi nyeupe
Magari yenye vibao vya rangi nyeupe vinavyoanza na herufi T yamesajiliwa kwa ajili ya matumizi ya kibiashara (Commercial Use). Mfano wa magari haya ni daladala, teksi, na magari ya huduma kama Bolt au Uber.
Hii inamaanisha kuwa gari hili linaruhusiwa kusafirisha abiria au mizigo kwa malipo.
Magari ya Serikali za Mitaa na mashirika ya umma
Magari haya yanatambuliwa kwa herufi maalum kama SM, SU, STK, STJ, au STL, ambapo SM hutumika kwa magari ya Serikali za Mitaa, mfano magari ya Halmashauri, SU hutumiwa na mashirika ya umma kama TANESCO au DAWASA na herufi STK, STJ, STL hutumiwa na maofisa wa Serikali Kuu, mfano wizara na idara za Serikali.
Magari ya wanadiplomasia na wafadhili
Magari yenye vibao vya namba za usajili zenye herufi DFP au DFPA hutumiwa kwenye miradi inayofadhiliwa na wafadhili wa kimataifa (Donor Funded Projects). Wanadiplomasia na wafadhili mara nyingi hutumia magari haya kwa shughuli za kidiplomasia, misaada au miradi maalumu ya maendeleo inayofadhiliwa na mashirika au taasisi za kimataifa.
Hata hivyo, magari yanayotumiwa na wanadiplomasia wa kikanda wa mashirika ya kimataifa hayo huwa na kibao chenye rangi ya bluu inayoanza na herufi T ikifuatiwa na CD.
Magari ya mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN)
Magari ya Umoja wa Mataifa yana vibao vya rangi ya bluu vinavyoanza na herufi T, ikifuatiwa na herufi CD. Hii inaonyesha kuwa gari hilo linamilikiwa na shirika mojawapo la Umoja wa Mataifa kama vile Shirika la Afya Duniani (WHO) au Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto (UNICEF).
Magari ya ofisi za ubalozi
Magari haya yana vibao vya rangi ya kijani yanayoanza na herufi T, ikifuatiwa na CD. Hii inamaanisha kuwa gari hilo linamilikiwa na ubalozi wa nchi fulani, mfano Ubalozi wa Marekani.
Magari ya majeshi ya ulinzi na usalama
Magari ya majeshi yana vibao vya rangi nyeusi, kijani, nyekundu au njano vyenye herufi JW au PT, ZT, au MT ambapo JW humaanisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) PT humaanisha Polisi Tanzania , ZT humaanisha Zimamoto Tanzania na MT humaanisha Magereza Tanzania wakati idara ya uhamiaji wao gari zao huwa na kibao kilichoandikwa UT.
Magari ya viongozi wa nchi
Viongozi wa kitaifa hutumia vibao vya rangi ya njano vilivyo na nembo ya Taifa pamoja na herufi kama W, NW, RC, na CAG. Hii inaashiria cheo cha mtumiaji wa gari hilo:
WM: kumaanisha Waziri wa Maji , NW: Naibu Waziri, RC: Mkuu wa Mkoa (Regional Commissioner), CAG: Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (Chief Auditor General).
Magari ya viongozi wa mahakama
Magari haya yanatumia vibao vya rangi ya njano pamoja na herufi kama JM, J, JK, na JR, ambapo JM humaanisha Jaji Mkuu, J ni Jaji wa Mahakama Kuu, JK ni Jaji Kiongozi na JR humaanisha Jaji wa Mahakama ya Rufaa.
Magari ya viongozi wa Bunge
Viongozi wa Bunge hutumia vibao vya rangi ya njano na herufi S, NS, au KUB, ambapo S ni Spika wa Bunge, NS: Naibu Spika pamoja na KUB kumaanisha Kambi ya Upinzani Bungeni.
Utaratibu wa usajili wa vyombo vya moto kwa Tanzania hutolewa na kusimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kufuata sheria za usajili wa vyombo vya moto (Motor Vehicles Registration Regulations) kwa magari yanayosajiliwa kwa matumizi binafsi pamoja na matumizi ya biashara.
Pamoja na hayo utaratibu wa usajili wa namba za magari tofauti na yale ambayo husajiliwa kwa ajili ya matumizi binafsi na biashara, hutegemeana na taratibu za shirika au taasisi husika ambao lazima ukubaliwe na nchi.