Sababu za Caf kuahirisha Chan mpaka Agosti 2025
- Ni pamoja na kutoa muda wa kutosha kukamilisha miundombinu ya viwanja itayotumika.
Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetangaza kusogeza mbele fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (Chan) 2024 zilizokuwa zifanyike Tanzania, Kenya na Uganda kuanzia Februari Mosi hadi Februari 28, 2025 na sasa zitafanyika Agosti 2025.
Taarifa iliyotolewa na CAF Jumanne, Januari 14, 2025 imeeleza kuwa kuahirishwa kwa Chan ni kutoa muda wa kukamilisha miundombinu kwa nchi waandaaji.
“Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) leo limetangaza kuahirishwa kwa Mashindano ya Mataifa ya Afrika ya TotalEnergies CAF (CHAN) Kenya, Tanzania, Uganda 2024 hadi Agosti 2025,
…maendeleo mazuri yameonekana nchini Kenya, Tanzania na Uganda katika ujenzi na uboreshaji wa viwanja, uwanja wa mafunzo, hoteli, hospitali na miundombinu mingine na vifaa kwa ajili ya mwenyeji wa mafanikio wa TotalEnergies African Nations Championship (CHAN) Kenya, Tanzania, Uganda 2024,” imeeleza taarifa ya Caf.
Hata hivyo, taarifa hiyo iliyochapishwa kwenye kurasa za Caf pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imebainisha kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kupokea ushauri wa wataalam wa wa ufundi na miundombinu wa CAF ambao baadhi yao wamekuwepo Kenya, Tanzania na Uganda kutaka muda wa matengenezo na ukarabati uongezwe zaidi.
Kwa upande wake rais wa shirikisho hilo, Patrice Motsepe amewashukuru Marais wa Tanzania, Kenya na Uganda kwa juhudi zao na uungaji mkono kwa maandalizi ya mashindano hayo.
“Ningependa kutoa shukrani za dhati kwa Rais William Ruto wa Kenya, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais Yoweri Museven wa Uganda kwa uongozi wao, kujitolea na maendeleo mazuri ambayo yamefanywa katika ujenzi na kuboresha viwanja, uwanja wa mafunzo, hoteli, hospitali na miundombinu mingine na vifaa,” amesema Motsepe.
Motsepe ameongeza kuwa ameshangazwa na ujenzi unaoendelea na ukarabati wa miundombinu ya soka na vifaa katika nchi hizo ambapo amesisitiza kuwa anaamini ifikapo Agosti 2025, miundombinu itakuwa imekamilika tayari kwa kuziwezesha nchi hizo kuandaa Chan.
Fainali za Chan hufanyika kila baada ya miaka miwili na awamu hii inashirikisha nchi 19 na kuahirishwa kwake kunatoa nafasi sio tu kwa nchi kuandaa miundombinu iliyosalia bali kutengeneza timu bora zaidi itayopaisha viwango vya Tanzania kimataifa.