Polisi yaua majambazi waliovaa nguo za kike Mwanza
- Ni baada ya kukataa kutii amri ya polisi ya kujisalimisha.
- Walivaa mavazi ya kike kuficha utambuzi wa jinsia na sura zao.
Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limewaua wanaume wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi baada ya watu hao kuvamia nyumbani kwa mfanyabiasha Flora Sungura Abdallah (42) Mkazi wa Mtaa wa Kabambo Wilaya ya Ilemela kwa lengo la kufanya uhalifu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Januari 10, 2025 amesema watu hao waliovaa mavazi ya kike kwa lengo la kuficha jinsia na mwonekano wao waliuawa jana Januari 9,2025 majira ya saa 2.45 usiku kwa kupigwa risasi na askari polisi waliokuwa wakifanya doria maeneo hayo.
“Watu hao walikuwa na bunduki aina ya shortgun moja iliyotengenezwa kienyeji ikiwa na risasi mbili na mapanga mawili ambapo walifanikiwa kuingia ndani wakati mfanyabiashara huyo amefunguliwa geti akitoka kwenye shughuli zake za kibiashara,”amesema Mutafungwa.
Kwa mujibu wa Mutafungwa baada ya watu hao kuingia ndani ya nyumba hiyo, wakazi wa eneo hilo walipiga kelele za kuomba msaada na taarifa hizo kufika kwa askari wa Jeshi la Polisi waliokuwa doria eneo hilo.
Mutafungwa amesema askari walifika kwa haraka kwenye eneo hilo kutoa msaada na kuwataka watu hao kujisalimisha kwa lakini walikaidi amri na kutaka kuwadhuru wakazi wa nyumba hiyo pamoja na askari.
“Kitendo hicho kilisababisha askari kufyatua risasi na kusababisha watu hao ambapo mmoja alishika bunduki na mwingine panga kujeruhiwa kwa risasi na kupoteza maisha papo hapo,” amesema Mutafungwa
Katika tukio hilo silaha aina ya Shortgun moja, mapanga mawili na begi la mgongoni likiwa na nguo suruali, shati, bisibisi na viatu vimepatikana kwenye eneo la tukio.
Hata hivyo, Mutafungwa amebainisha kuwa watu wengine wawili wa jinsia ya kiume ambao walikuwa ni washiriki katika tukio hilo walifanikiwa kutoroka kwa pikipiki ambayo haijasajiliwa na kwamba msako unaendelea ili kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria.
Mutafungwa amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwafichua wahalifu na uhalifu na akiwasisitiza wafanyabiashara kuweka kamera za ulinzi kwenye makazi yao na maeneo ya biashara ili kurahisisha jitihada za jeshi hilo katika kuwadhibiti wahalifu.
Miili ya watu hao ambayo haijatambuliwa imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa Bugando ikisubiri utaratibu wa utambuzi na uchunguzi wa kitaalamu.
Katika tukio jingine, mtu mmoja moja mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20 hadi 25 amefariki dunia huku wengine wanne kujeruhiwa kufuatia ajali iliyohusisha gari aina ya Toyota Coster ikitokea Nyegezi kuelekea Mwanza mjini kugongana na gari Toyota IST kisha kuigonga hiace liyokuwa ikitokea Mwanza mjini kuelekea Nyegezi.
Ajali hiyo imetokea leo Januari 10, 2024 katika barabara ya Kenyatta eneo la Iseni kata ya Butimba baada ya dereva wa gari aina ya Toyota Coster kutaka kuyapita magari mengine sehemu isiyoruhusiwa bila kuchukua tahadhari.
Waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo ambao wamelazwa hospital ya Rufaa ya Kanda Bugando ni pamoja na Maua Rashid (30) mkazi wa Buhongwa, Fabiani Ndalo (50), Hadija Mussa (24) makazi wa kiloleli na David Mussa (27) mkazi wa Kiseke ‘A’
“Jeshi la polisi limeanza msako wa kumtafuta dereva aliyetoroka eneo la tukio baada ya kusababisha ajali ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria,”amesema Kamanda Mutafungwa.