Jinsi unavyoweza kupunguza maumivu ya ada Januari
- Ni pamoja na kujiandaa mapema na kufungua akaunti za akiba kwa watoto.
Arusha. ‘Mwezi dume’ ndivyo baadhi ya watu huuita mwezi Januari ambao kikawaida hukabiliwa na majukumu mengi ikiwemo ulipaji wa kodi za pango pamoja na ada kwa wanaosomesha.
Kwa wazazi na walezi mwezi wa watoto wanaosoma shule binafsi huu ndio wakati wa ‘kukuna kichwa’ hususani tarehe za mwanzoni ambapo shule nyingi hufunguliwa ikiashiria kuanza kwa muhula mpya wa masomo.
Kiuhalisia ugumu wa mwezi Januari hutokana na kuwa umefuatana na mwezi wenye sherehe nyingi ambazo nazo huhitaji pesa kwa ajili ya vyakula, vinywaji, mavazi pamoja na zawadi.
Wakati huo huo katika baadhi ya maeneo huwa msimu wa kilimo mwezi huo, hivyo wakulima hulazimika kutoboa mifuko yao kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya msimu mpya wa kilimo.
Hata hivyo, Januari itaendelea kuwepo na majukumu yataendelea kuwepo na huenda yakaongezeka, kinachotakiwa si kulalamika bali kutafuta njia bora ya kutimiza majukumu hitajika bila kuacha maumivu kwa wahusika.
Nukta habari imezungumza na wazazi, walimu na washauri wa masuala ya kifedha ambao wameanisha sababu na mbinu za kupunguza maumivu ya ada kipindi cha mwanzo wa Mwaka.
Kufanya maandalizi mapema
Baraka Ndoto, baba wa watoto wawili anasema ni vyema mzazi kuanza maandalizi ya ada mapema na kwa wenye kipato chini wanaweza kuanza mapema zaidi huku wakipunguza matumizi yasiyo ya lazima wakati wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
“Ukishajua unasomesha ni lazima ujipange, kwa wale wenye kipato cha chini unaweza kuanza mapema zaidi hata miezi sita kabla ya siku ya kulipa ada na ikitokea kuna sherehe pia unaweza kupangilia bajeti yake mapema,” amesema Baraka.
Shabani Omary Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Kiislamu Arusha amesema kuwa kipindi hiki wao hupokea simu za mara kwa mara kutoka kwa wazazi ambao hawakujipanga kulipa ada mapema kuomba watoto wao waingie shule jambo ambalo linaleta usumbufu kwa walimu na wanafunzi,
Ametaja umuhimu wa ada kulipwa mapema kuwa ni pamoja na kuzoea mazingira kwa wale wanaoingia ngazi mpya ya elimu ikiwemo kidato cha kwanza.
“sisi tumefungua shule Januari 7, 2024 ili wanafunzi wapya na wale wa bweni wapate nafasi ya kuzoea mazingira na kujiandaa kisaikolojia kwa ajili ya muhula mpya wa masomo,” amesema Mwalimu Shabani.
Mbali na ada wazazi wanashauriwa kuanza maandalizi mengine mapema ikiwemo nguo za shule, viatu na madaftari.Picha|Lucy Samson.
Kuipa kipaumbele elimu ya mtoto
Lawrence Gimirey, Mwalimu Mkuu Mstaafu kutoka Shule ya Msingi Ngarasero iliyopo jijini Arusha ameiambia Nukta habari kuwa miongoni mwa sababu za wazazi kutokulipa ada mapema ni kutoipa elimu ya mtoto kipaumbele.
Amesema mzazi mwenye akili anayefahamu umuhimu wa elimu ya mtoto wake ni lazima atajipanga mapema kuhakikisha mtoto anakuwepo darasani tangu siku ya kwanza masomo yanapoanza.
“Mazazi ni lazima ujue kuwa unasomesha watoto wangapi, nani yupo shule gani, ada yake ni shilingi ngapi na utailipaje kabla ya wakati kufika kinyume na hapo utakuwa huthamini wala kuipa kipaumbele elimu,” amesema Gimirey.
Kufungua akaunti za akiba kwa watoto
Mshauri wa masuala ya fedha CPA(T) Fadhili Agustino ameshauri wazazi kufungua akaunti za akiba kwa ajili ya masomo ya watoto ili kukabiliana ukata kipindi cha Januari.
“Ukifungua hizi akaunti itakusaidia pale ambapo utakwama unaweza kuchukua kidogo na kulipia ada na hii inasaidia sana kupunguza mawazo kwa wazazin kipindi hiki,” amesema Agustino.
Mshauri huyo ametolea mfano akaunti ya NMB mtoto akaunti unayoweza kumfungulia mtoto tangu akiwa na siku moja mpaka akiwa na miaka 17.
Kulipa ada kwa awamu
Baadhi ya shule huruhusu kulipa ada za watoto wao kwa awamu jambo linalopunguza maumivu kwa wazazi au walezi katika mwanzo mpya wa mwaka.
Mathalan katika shule ya Arusha Boys, mwalimu Shabani anasema wanapokea malipo kwa awamu nne ili kuwawezesha wazazi kumudu gharama hizo za elimu kwa watoto wao.