Nane wafariki dunia katika ajali ya gari Tanga

December 24, 2024 4:46 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Sababu ya ajali hiyo ni dereva wa Coaster kushindwa kulimudu gari lake na kugongana uso kwa uso na lori la mizigo.
  • Watu 8, wanaume 5 na wanawake 3 wamefariki katika ajali hiyo.

Dar es Salaam. Watu nane wamefariki dunia na wengine nane kujeruhiwa kwenye ajali iliyotokea leo Desemba 24, 2024, majira ya saa 11:00 asubuhi, katika Kitongoji cha Kwachuma, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga.

Taarifa ya Almachius Mchunguzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga iliyotolewa leo Disemba 24, 2024 inafafanua kuwa  chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari aina ya Toyota Coaster, Thomas Hunay Gidahonda (33)  kushindwa kulimudu gari lake hali iliyosababisha kuyumba na kugongana uso kwa uso na lori la mizigo na kusababisha watu hao kupoteza maisha.

“Kwa bahati mbaya (ajali hiyo) imesababisha vifo vya watu nane, wanaume watano, wanawake watatu na Majeruhi nane,” imesema taarifa ya Mchunguzi.

Majeruhi katika ajali hiyo ni pamoja na Godlisen Hamphrey Minja (20), mfanyabiashara na mkazi wa Mabibo Dar es salaam, Riziki Mboya(28), dereva na mkazi wa Njiapanda Moshi, Lina Victus Swai (25), mfanyabiashara, Gospan Wingod Lema, (24) fundi umeme na mkazi wa Temeke Dar es Salaam.

Wengine ni Loyce Nuhu James, (27) mkazi wa Buguruni Dar es Salaam, Lucy Mathew Urio, (24) mkazi wa Dar es salaam na majeruhi wawili wa lori ambao ni dereva wa lori Yona Stephano Madandi, (35) mkazi wa Goba Dar es salaam na utingo wake Samweli Adinani Hossen, (24), mkazi wa Dar es salaam.

Ajali hiyo imetokea siku chache mara baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa kutoa angalizo kuzingatia sheria za barabarani tunapoelekea sikukuu za mwisho wa mwaka. 

Akizungumza na waandishi wa habari Disemba 18, 2024 Bashungwa alitoa wito kwa wasafiri na wasafirishaji kuzingatia na kuheshimu sheria hizo ili kupunguza ajali zinazoepukika ili kuepusha vifo, majeraha au ulemavu utokanaona ajali za barabani.

“Yapo matukio ya ajali ambazo zinatokana na uzembe wa madereva,ama wamiliki wa magari kutofanyia matengenezo mara kwa mara vyombo vyao vya usafiri” amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa alitoa onyo kwa madereva wenye tabia ya kuendesha mwendokasi, kujaza abiria kupita kiasi na wote wanaotumia vileo kisha kuendesha vyombo vya moto kuweza kuacha tabia hizo mara moja na kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks