Tahadhari za kiusalama za kuchukua sikukuu za mwisho wa mwaka

December 25, 2024 9:00 am · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Usiwaache watoto pekee yao.
  • Linda mali zako unapokuwa kwenye mkusanyiko wa watu.
  • Shirikiana na vyombo vya usalama kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu.

Dar es Salaam. Msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, Krismas na Mwaka Mpya, watu wengi hujumuika pamoja na familia, marafiki, na jamaa zao kusherehekea kwa furaha na shangwe.

Hata hivyo, wakati huu hukumbwa na changamoto za usalama kutokana na msongamano wa watu, magari. 

Pia matukio mbalimbali ya kijamii yanayoandaliwa maeneo ya starehe, fukwe za bahari, migahawa, na sehemu za manunuzi yanaweza kuchangia usalama wa watu kupungua kama hakuna usimamizi mzuri.

Jeshi la Polisi hutoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari za ziada kuhakikisha usalama wao, hasa kwa watoto wadogo, ambao mara nyingi wako hatarini zaidi wakati wa shamrashamra za sikukuu.

Zingatia mambo haya ili kuimarisha usalama wako binafsi na wale wanaokuzunguka katika msimu huu wa sikukuu:

Hakikisha watoto hawatoweki kutoka katika uangalizi wa watu wazima wanapokuwa maeneo ya mikusanyiko. Ni muhimu kuwapa watoto namba za simu za dharura kwa ajili ya mawasiliano pindi inapotokea tatizo.

Unaweza kumpa mtoto vitambulisho rahisi, kama kadi au bangili yenye taarifa muhimu, ikiwa ni pamoja na majina ya wazazi na namba ya simu, ili kuhakikisha upatikanaji wa mtoto wako kwa haraka na urahisi pale inapotokea amepotea.

Wazazi kuwa karibu na watoto wao wanaposherehekea kunawafanya watoto kuwa salama zaidi. Picha| 123rf.com

Unaposherehekea na kufanya matembezi kwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya kustarehe, epuka kwenda katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu na magari, kwani yanaweza kuwa mazingira rahisi kwa uhalifu kutokea.

Kwa madereva wa vyombo vya moto ni muhimu kuzingatia matumizi sahihi ya barabara wanapokuwa wanaendesha. Zingatia alama za barabarani, epuka mwendokasi na kilevi. Hii itasaidia kuepusha ajali na vifo vya watu.

Katika masoko na maduka makubwa, watu wanatakiwa kuwa waangalifu na mifuko yao ya fedha, hasa wanawake wanaobeba pochi, ili kuepuka wizi wa mkupuo.

Waziri wa Mambo ya Ndani,Innocent Bashungwa akizungumza na waandishi wa habari Desemba 18, 2024 alitoa angalizo kwa madereva, wasafiri pamoja na wazazi na walezi kuzingatia usalama tunapoelekea sikukuu za mwisho wa mwaka Krismas na Mwaka Mpya. 

Bashungwa aliwataka wasafiri na wasafirishaji kuzingatia na kuheshimu sheria za usalama barabarani kupunguza ajali zinazoepukika ili kuepusha vifo, majeraha au ulemavu utokanaona ajali za barabani.

“Yapo matukio ya ajali ambazo zinatokana na uzembe wa madereva, ama wamiliki wa magari kutofanyia matengenezo mara kwa mara vyombo vyao vya usafiri,” alisema Bashungwa.

Unywaji wa pombe wakati unapoendesha chombo cha moto ni hatari kwa usalama barabarani. Picha| Caranddriver.com

Wananchi wanashauriwa kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za viashiria vya kihalifu mapema kwani usalama wa jamii ni jukumu la kila mmoja. 

Kwa tahadhari hizi, wananchi wanaweza kusherehekea Krismasi na Mwaka Mpya kwa furaha na amani, huku wakiweka mbele usalama wa familia na jamii kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks