Sababu maafisa wanafunzi wa jeshi 59 kushindwa kuhitimu
- Ni pamoja na kushindwa kufikia viwango vya kitaaluma vilivyowekwa.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu amewatunuku kamisheni maafisa wanafunzi 236 waliohitimu mafunzo ya kijeshi huku wengine 59 wakishindwa kuhitimu kwa sababu mbalimbali ikiwemo kushindwa kufikia viwango vya kitaaluma vilivyowekwa.
Wahitimu hao ni wale waliopata mafunzo katika chuo cha kijeshi cha Tanzania (TMA) kwa miaka mitatu kwa wanafunzi wa kundi la 5/21 waliosoma shahada ya sayansi ya kijeshi kuanzia Novemba 8, 2021 na kundi la 71/23 ‘regular’ lilioanza kozi hiyo Novemba 27, 2023 na kuhitimu leo.
Kati ya maafisa wanafunzi 236, waliohitimu leo wanaume ni 203 na wanawake 33 ambao wanaanza rasmi safari ya kulitumikia Taifa katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mpaka pale watakapostaafu.
Brigedia Jenerali Jackson Mwaseba, Mkuu wa chuo hicho aliyekuwa akizungumza katika mahafali ya wahitimu hao yaliyofanyika leo Novemba 27, 2024 jijini Arusha amesema kuwa sababu za wanafunzi hao kushindwa kuhitimu zimegawanyika katika makundi mawili kulingana na mwaka walioanza masomo.
Kwa mujibu wa Brigedia Mwaseba kundi la 5/21 shahada ya sayansi ya kijeshi lililoanza mafunzo Novemba 8, 2021 lilikuwa na jumla ya wanafunzi 101, kati yao wanafunzi 74 pekee ndio waliotunukiwa kamisheni huku wengine 26 wakishindwa kuhitimu kutokana na sababu nane tofauti.
Walioachishwa mafunzo ni 26 kwa sababu mbalimbali za maombi binafsi, utovu wa nidhamu, mwenendo wa tabia isiyoridhisha, kutofikia viwango vya kitaaluma, kukosa uaminifu, ugonjwa, utoro huku maafisa wanafunzi watatu walihitajika makao makuu ya jeshi kwaajili ya kufanya taratibu za kwenda kufanya mafunzo nje ya nchi.
Maafisa wanafunzi wakivalishana vyeo baada ya kutunukiwa Kamisheni na Rais Samia Suluhu Hassan, katika hafla iliyofanyika leo Novemba 28, 2024 kwenye Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi (TMA) Monduli, jijini Arusha. Picha| Ikulu
Kundi lingine ni 71/23 ‘Regular’ walioanza kozi Novemba 27, 2023, ikiwa wakiwa 128, wanafunzi 21 kati yao wakitokea nchi rafiki za Eswatini, Kenya, Malawi, Rwanda, Uganda, Msumbiji na Zambia.
Hata hivyo, wanafunzi 33 hawakuhitimu kwa sababu nane ikiwemo kukimbia mafunzo na kukosa utimamu wa mwili.
Walioachishwa mafunzo ni wanafunzi 33 kwa sababu mbalimbali za wanne kukimbia mafunzo, mmoja kukosa utimamu wa mwili, mmoja kukosa uaminifu, wagonjwa saba, kumi na mbili kutofikia viwango vya kitaaluma na wawili wenye tabia isiyoridhisha.
Kosa jingine ni kukosa nidhamu kwa mmoja huku mwanafunzi mwingine mmoja akifariki wakati wa mafunzo. Hivyo kufanya maafisa wanafunzi 74 Watanzania kutunukiwa kamisheni na kuwa maafisa wa jeshi leo.
Mafunzo nje ya nchi
Kundi la tatu lilikuwa na maafisa wanafunzi 88 waliopata mafunzo nje ya nchi ikiwemo Urusi, Kenya, Msumbiji, Burundi, Uganda, China, Misri, Ethiopia, India, na Zambia.
Maafisa wanafunzi hao wamehitimu bila changamoto yoyote na walijiunga chuoni hapo kwa maandalizi ya kutunukiwa kamisheni.