Uchaguzi Serikali za mitaa waisha kwa sura tofauti

November 27, 2024 6:49 pm · Waandishi Wetu
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam kukiwa na watu wengi na kwingine kukiwa na wachache waliojitokeza kupiga kura.

Dar es Salaam. Upigaji kura kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa na vijiji nchini umehitimishwa jioni ya leo huku katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam kukiwa na watu wengi na kwingine kukiwa na wachache waliojitokeza kupiga kura. 

Waandishi wa Nukta Habari waliotembelea maeneo mbalimbali katika manispaa za Ubungo, Kinondoni, Temeke na Jiji la Dar es Salaam wameshuhudia baadhi ya vituo vilikuwa na muutikio mkubwa wa wapiga kura tangu asubuhi lakini vingine vikikosa watu kwa zaidi ya dakika 15. 

Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais-Tamisemi Watanzania milioni 31.2 walikuwa wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu ikiwa ni sawa na asilimia 94.8 ya watu wenye umri wa kupiga kura. 

Waziri wa Ofisi ya Rais- Tamisemi, Mohammed Mchengerwa amesema matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa ndani ya 72 ambapo miongoni mwa takwimu zinazotarajiwa ni mwitikio wa watu waliojitokeza kupiga kura. 

Katika kituo cha Ulongoni A Mtaa wa Mongolandege jijini Dar es Salaam mpaka kufikia majira ya saa 5:20 asubuhi idadi ya waliojitokeza ilikuwa ndogo na hata maeneo waliokuwa wametengewa kwa ajili ya kusubiri mchakato ukiendelea yalikuwa wazi.

Hali ilikuwa hivyo hivyo katika Kituo cha Bangulo Shule ya Sekondari kata ya Pugu. Mwitikio katika kituo hicho haukuwa mkubwa sana hadi kufika majira ya saa 4:26 muitikio wa watu ulikuwa mdogo huku wengine wakionekana kuendelea na majukumu yao ya kila siku.

Katika eneo la Kinyerezi Shule majira ya saa sita mchana nako kulikuwa na idadi ndogo zaidi ya watu ukulinganisha na maeneo mengine.

Msimamizi wa uchaguzi katika kituo cha uchaguzi cha Kinyerezi jijini Dar es Salaam ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema sababu kubwa ya watu kutokujitokeza ni pamoja na kutokea kwa msiba wa mzee maarufu katika eneo hilo.

Hata maeneo ya Uswazi

Baadhi ya vituo vingine vilivyopo kwenye maeneo yenye wakazi wengi navyo vilikuwa na watu wachache waliojitokeza kupiga kura ikiwemo Tandale katika Manispaa ya Kinondoni. 

Katika kituo cha kupigia kura Mtaa wa Pakacha, Tandale ambapo mpaka majira ya saa nne asubuhi wakati mwandishi wa Nukta anafika eneo hilo kulikuwa na wapiga kura wachache wanaoonekana eneo hilo.

Mmoja ya mpiga kura Mussa Ramadhan amesema huenda kutoonekana kwa majina ya waliojiandikisha katika karatasi zilizobandikwa kituoni ikawa sababu ya idadi ya watu kuwa ndogo.

“Tulishazoea zile karatasi zinazopigwa ‘photocopy’ ambazo majina yanaonekana vizuri lakini sio hizi majina ni changamoto kuyaona hadi uombe uhakikiwe kwenye kitabu,” amesema Ramadhan.

Katika Kituo cha upigaji kura Shule ya Msingi Mloganzila iliyopo katika kijiji cha Mloganzila, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani na kushuhudia idadi ndogo ya watu wa eneo hilo wakijitokeza kupiga kura.

Kituo cha Mzimuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa vituo vilivyokuwa na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kupiga kura leo. Picha|Esau Ng’umbi/Nukta.

Vijana siyo kivile

Tofauti na vituo vingine ambavyo wapiga kura hupanga foleni, katika kituo cha Shule ya Msingi Mloganzila wasimamizi walilazimika kusubiri dakika kadhaa baada ya mpiga kura mmoja kufanikisha zoezi la upigaji kura ndipo mpiga kura mwingine ajitokeze kupiga kura.

Sehemu kubwa ya waliojitokeza ni watu wa umri wa makamu na wazee huku kukiwa na vijana wachache. 

Mkazi wa Mloganzila Ambros Magabe (81), aliyejitokeza kupiga kura mapema katika kituo hicho, amesema kuwa ameshangazwa kuona hakuna kijana aliyejitokeza kupiga kura katika eneo hilo na badala yake wazee kama yeye ndiyo wamekuwa na mwamko wa kupiga kura.

“Makosa yanafanyika hasa kwa vijana, hawaji kupiga kura halafu baadae wanasema, yule hafai. Kama hafai si ungeenda kupiga kura ukaseme hapana,” amesema mzee Magabe.

Katika wilaya hiyo hiyo ya Kisarawe mkoani Pwani, katika kituo cha upigaji kura Ofisi ya Kata ya Kiluvya, majira ya saa saba mchana Nukta ilifika na kushuhudia uwepo wa askari pamoja na waratibu wa zoezi la upigaji kura tu bila ya kuwepo mpiga kura hata mmoja katika eneo hilo.   

Katika Kituo cha kupigia kura cha Bangulo CCM kulikuwa na idadi ndogo ya watu waliojitokeza kupiga kura siku ya leo. Picha|Fatuma Hussein/Nukta.

Ugumu wa kusaka majina watajwa 

Kuna hofu kuwa ugumu wa kutafuta majina kumewakimbiza wengi kushiriki kupiga kura. 

Baadhi ya waliowahi mapema ili kutafuta majina yao na kuyakosa kwa wakati sambamba na kukosa usaidizi wa kuyatafuta wamehairisha kupiga kura na kusema watakwenda kwa muda mwingine kabla ya muda wa kituo kufungwa.

“Kuna wengine ni watu wazima, usumbufu wa kutafuta jina kwa muda mrefu hawawezi, wasiposaidiwa wanashindwa kupiga kura wanaondoka,” amesema Agatha Wanderage mkazi wa Pugu Sekondari.

Hata hivyo, kuna vituo ambavyo watu wamejitokeza kwa wingi kupiga kura vikiwemo vya Yangeyange, Msongola, Kibamba, na Bangulo Shule ya Msingi ambacho wapiga kura walianza kupiga kura Saa 4:00 bila sababu ya msingi. 

Uchaguzi umehitimishwa kukiwa na malalamiko lukuki kutoka kwa upinzani juu ya uwepo wa kura zilizopigwa huku vyombo vya dola vikakamata baadhi ya watuhumiwa wakiwemo waliokimbia na sanduku lenye kura 181.

Habari hii imeandaliwa na Davis Matambo, Kelvin Makwinya, Esau Ng’umbi na Fatuma Hussein. Kwa maoni tuma kwenda newsroom@nukta.co.tz.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks