Wakosa majina uchaguzi wa Serikali za mitaa
- Ukosefu wa majina katika orodha ya wapiga kura yawakwamisha kupiga kura Serikali za mitaa.
- Baadhi wasusa na kuondoka jambo lililowanyima fursa ya kupiga kura.
Dar es Salaam/Mwanza/Arusha. Baadhi ya wakazi wa mitaa na vijiji mbalimbali nchini wamelalamikia kutoona majina yao katika orodha ya wapiga kura huku wengine wakikosoa utaratibu wa kupanga majina bila mpangilio rafiki.
Vituo vya kupigia kura za kuchagua viongozi wa Serikali za mitaa vyote vinatakiwa kubandikwa majina nje ili kuwawezesha wapiga kura kuyaona kwa haraka kufahamu eneo halisi wanalotakiwa kupigia kura.
Watanzania leo Novemba 27 wanapiga kura kuwachagua viongozi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji watakaowangoza kwa miaka mitano mingine.
Baadhi ya waliokosa majina yao wameiambia Nukta Habari kuwa wametumia muda mwingi kusaka majina yao bila mafanikio jambo lililofanya wakate tamaa na kuondoka.
Mkazi wa Mtaa wa Yangeyange kata ya Msongola katika Jiji la Dar es Salaam Mwita Benjamin amesema alifika kwenye kituo cha kupikia kura Saa 4 asubuhi lakini hadi alitafuta jina lake zaidi ya saa moja na nusu bila mafanikio.
“Majina hapa hayajakaa kimpangilio, yamechanganywa tarehe za kujiandikisha na ni ngumu sana kwa mpiga kura kuona jina lake kirahisi. Nimelikosa jina langu kwa sasa nimeamua niondoke nikipata muda na nguvu tena nitarudi,” amesema Mwita.
Katika kituo cha kupigia kura cha Mtaa wa Yangeyange kilichopo katika Shule ya Msingi Msongola baadhi ya wakazi wamekosa majina yao licha ya kujiandikisha akiwemo mmoja wa wanahabari wa kampuni ya Nukta Africa.
Mpaka tulipate: Wakazi wa Mtaa wa Kibamba katika Manispaa ya Ubungo wakipitia karatasi zenye orodha ya majina ya wapiga kura. Baadhi wamelalamikia karatasi hizo kutopangwa kwa mpangilio mzuri. Picha|Kelvin Makwinya/Nukta.
‘Jina langu limeenda wapi?’
Mkazi wa Kibamba katika Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina moja la Judith amesema tangu aanze kupiga kura hajawahi kushuhudia uchaguzi wenye usumbufu kama wa mwaka huu.
“Nimekuja na rafiki yangu ambaye nilifatana naye wakati wa uandikishaji lakini jina lake lipo na langu hakuna. Jina langu limeenda wapi?,” amehoji.
Juma Khamis, mkazi mwingine wa Kibamba amesema vituo vya kupiga kura vimewekwa mbalimbali kiasi kwamba anayekosa kuona au kusikia jina lake likiitwa na wasimamizi wa uchaguzi anajikuta akihaha kutembea kutoka eneo moja kwenda jingine bila mafanikio.
Mkoani Mwanza nako baadhi ya waliojiandikisha kupiga kura wameyakosa majina yao jamboi lililozua taharuki na kuwakatisha tamaa.
Baadhi ya wakazi katika Mtaa wa Ugunja kata ya Mirongo wamefika katika kituo cha kupigia kura na kukuta majina yao hayapo kwenye orodha ya majina ya wapiga kura licha ya kujiandikisha.
Mmoja wa wasimamizi wa uchaguzi katika kituo cha Shule ya Msingi Kinyerezi katika kata ya Kinyerezi jijini Dar es Salaam ambaye hakutaka kutajwa jina amesema kwenye kituo chake hakuna waliokosa majina kwa kuwa idadi ya waliojitokeza ni ndogo na matarajio.
Baadhi ya wapiga kura waliojitokeza kupiga kura katika Mtaa wa Kasese kata ya Mkolani jijini Mwanza licha ya mvua kubwa iliyonyesha mkoani humo asubuhi ya leo. Picha|Yuster Massawe/Nukta.
Bora nirudi ‘home’
“Nilijitokeza kujiandikisha ili nimchague kiongozi atakayeniongoza kwa miaka mitano lakini nimefika hapa naangalia jina langu silioni hivyo nimeamua kurudi nyumbani nikaendelee na shughuli zingine,” amesema Anicia Charles Mkazi wa mtaa wa Ugunja jijini Mwanza.
Mkazi mwingine Hussein Katabazi pia hakufanikiwa kutimiza haki yake ya msingi baada ya jina lake kutoonekana kwenye orodha ya majina ya wapiga kura.
Katabazi amesema yeye ni mtu wa nne kati ya anaowafahamu ambao wamekosa majina yao kwenye orodha hiyo.
Mkuu wa Mkoa ww Mwanza, Said Mtanda amewataka wakazi wa mkoa kujitokeza kupiga kura kwa kuwa uchaguzi utafanywa kwa uhuru na haki.
Atakayeshinda, ndiyo atatangazwa
Mtanda amesema makubaliano katika mkoa huo ni kwamba mgombea atakayeshinda ndiye atakayetangazwa.
Hali hiyo imeshuhudiwa katika baadhi ya vituo vya jiji la Arusha kaskazini mwa Tanzania ambapo baadhi ya wapiga kura wamelalamikia maandishi kwa madogo, kufutika ama kutoona kabisa majina yao.
Katika kituo cha kupiga kura cha Mtaa wa Mlimani kata ya Muriet jijini Arusha wananchi wa eneo hili wamejitokeza kupiga kura huku wengine wakilalamikia orodha ya majina yao yaliyobandikwa ukutani kutoonekana vizuri au kutokusomeka kabisa.
Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Mlimani, kata ya Muriet jijini Arusha wakisaka majina yao kabla ya kupiga kura asubuhi ya Novemba 27, 2024. Baadhi wamekosa majina na kurejea makwao. Picha|Lucy Samson/Nukta.
Mwandishi wetu ameshuhudia baadhi yao watu wakiondoka eneo hilo bila kupiga kura kama walivyokuwa wamepanga.
Wakati baadhi wakilalamikia kukosa majina yao kwenye orodha ya wapiga kura, wengine wamepiga kura vizuri ndani ya muda mfupi licha ya kutumia muda mrefu kuyasaka majina yao.
Hadija Sulum, mkazi wa Mtaa wa Yangeyange kati ya Msongola jijini Dar es Salaam amesema amefanikiwa kupiga kura baada ya kuliona jina lake. Mama huyo alitumia zaidi ya Saa moja kuona jina lake katika eneo hilo la kusini mwa mkoa wa Dar es Salaam.
“Changamoto ni majina, majina hayakuwekwa kwa mpangilio wa herufi, yamechanganywa changanywa ndio maana watu wengi bado wako pale, mimi nimetumia kama nusu saa kutafuta jina na kupiga kura,” amesema Shakira Yusuf, Mkazi wa Mtambani Manda B, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Habari hii imeandikwa na Fatuma Hussein, Kelvin Makwinya, Esau Ng’umbi, Nuzulack Dausen wakiwa Dar es Salaam, Lucy Samson (Arusha) na Mariamu John akiwa Mwanza.