Rais Samia: Maamuzi yenu katika sanduku la kura yataheshimiwa

November 26, 2024 6:50 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ametaka sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi kuzingatiwa.
  • Aeleza vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa mbili asubuhi na kufungwa saa 10 jioni.

Dar es Salaam. Kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,2024, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaeleza wananchi kuwa maamuzi yao katika masanduku ya kupigia kura yataheshimiwa.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza na wananchi Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma leo Novemba 26, 2024, ameongeza kuwa Watanzania wanapaswa kutumia fursa ya uchaguzi ili kuhakikisha wanawachagua viongozi waaadilifu, wabunifu na wenye maono ya kuongoza jamii za Kitanzania.

“Kumbukeni kila kura ina umuhimu mkubwa katika kuamua mustakabali wa maendeleo yetu na Taifa kwa ujumla,” amesema Rais Samia.

Hata hivyo, Rais Samia amewata viongozi wa vyama vya siasa, wagombea wa vyama vya uchaguzi na mawalaka wa uchaguzi kuzingatia na kuheshimu sheria na kanuni za uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa huru na wa haki.

“Nawasihi wasimamizi wa uchaguzi na wote wanaohusika na chaguzi hizo kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, uwazi na kwa kuzingatia taratibu zilizokubaliwa na wadau. Ni matumaini yangu mtaendelea kutekeleza majukumu yenu kwa weledi kwa  kuzingatia haki za wananchi na kudumisha utulivu tunapoelekea mwisho wa mchakato huu, ” ameeleza Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa vituo vya kupiga kura vipo kwenye mitaa na vitongoji vyote nchini kwenye majengo ya umma na maeneo ya wazi yaliyokubaliwa ambapo vituo vitafunguliwa kuanzia saa mbili asubuhi na kufungwa saa 10 jioni.

Uchaguzi wa Serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika wakati ambao bado kuna vuguvugu la kisiasa kutoka kwa upande wa vyama vya upinzani kushutumu huenda uchaguzi usiwe wa huru na wa haki.

Mathalani, Chama cha Demokrasia na Maendelea (CHADEMA)  kupitia kiongozi wao mkuu wa CHADEMA, Freeman Mbowe mnao Novemba 20, 2024 walitoa madai kwa vyombo vya habari kuwa wagombea wake wengi wameenguliwa kwa njia zisizo za haki kuwania katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa. 

Na kupitia taarifa iliyotolewa kwa wanahabari Novemba 12,2024, Waziri wa Tamisemi Mohamed Mchengerwa alieleza kuwa kwa kuzingatia mamlaka aliyonayo anaongeza muda wa kamati za rufani za wilaya wa kupokea, kusikiliza na kutoa uamuzi wa rufaa iliyowasilishwa kwa muda wa siku mbili zaidi hadi Novemba 15, 2024.

Mamlaka hayo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 52 ya Tangazo la Serikali Na.571,573, 574 na Kanuni ya 50 ya Tangazo la Serikali Na.572 yote ya tarehe 12/7/2024.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks