Wanne wafariki, 70 waokolewa ajali ghorofa la Kariakoo

November 16, 2024 9:00 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Muhimbili yaeleza kuwa majeruhi 35 ya 40 iliyowapokea wameruhusiwa baada ya ya kufanyiwa uchunguzi na kutibiwa 
  • Yaeleza kutopokea mwili uliotokana na ajali
  • Wengi ya waliokolewa ni vijana. 

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imetoa orodha ya majina 40 kati ya 70 waliojeruhiwa kwenye ajali ya kuporomoka kwa ghorofa Kariakoo, Jijini Dar es Salaam ambayo imeshagharimu maisha ya watu wanne huku wengine wakihofiwa kunaswa na vifusi 

Muhimbili imeeleza katika taarifa yake kuwa hadi kufikia saa 11 jioni majeruhi 35 kati ya 40 iliyokuwa imewapokea walikuwa wamesharuhusiwa kurejea makwao baada ya kufanyiwa uchunguzi na kutibiwa sehemu mbalimbali za mwili walizobainika kupata majeraha.

Sehemu  kubwa ya wamejeruhi hao kwa mujibu wa uchambuzi wa takwimu uliofanywa na Nukta Habari ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 19 na 35. 

Mkuu wa Mawasiliano kwa Umma wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, amesema majeruhi wengine watano wanaendelea na matibabu na kati yao wanne wamepelekwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa ajili matibabu zaidi.

Jengo hilo liliporomoka leo Novemba 16, 2024 majira ya saa tatu asubuhi ambapo kwa mujibu wa mashuhuda waliozungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania ( TBC) ndani ya jengo hilo la kibiashara, kulikuwa na wafanyabiashara na wateja kadhaa waliokuwa wakinunua bidhaa.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema watu wanne wamefariki dunia huku wengine 70 wakiokolewa kutoka kwenye ajali hiyo. 

Awali Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Peter Mtui, alisema watu watano walikuwa wamepoteza maisha kutokana na ajali hiyo, idadi inayotofautina na ile ya iliyotajwa na Chalamila. 

Chalamila amesema kuwa takwimu zaidi kuhusu ahali hiyo zitatolewa Saa 4.30 usiku Novemba 16. 

Hata hivyo, Muhimbili imesema haijpokea mwili wowote kutoka kweye ajali hiyo licha ya kuwa ni hospitali kubwa zaidi nchini. 

Vijana waokolewa zaidi

Uchambuzi wa orodha ya majina uliofanywa na Nukta Habari umebaini kati ya majeruhi waliopelekwa Muhimbili kwa matibabu, vijana ndio wengi zaidi wakiwa na wastani wa miaka kati ya 18 na 35 huku watatu tu ndio wenye umri wenye zaidi ya miaka 45. 

Mashuhuda hao wameeleza kuwa ghorofa hilo limeanguka ghafla majira ya saa 3:05 asubuhi wakati mafundi wa ujenzi walipokuwa kazini wakitoboa kwa ajili ya kuongeza sehemu ya maduka chini ya jengo hilo.

“Tulianza kusikia kelele za mtingishiko, kisha kwa ghafla jengo zima likaanguka, wananchi wameshindwa kujiokoa na kazi ya ujenzi ilianza tangu jana, hivyo angetaka urahisi angebomoa tu jengo lote,” amesema mmoja wa mashuhuda, Harrison Shayo.

Rais Samia atoa pole akiwa safarini

Muda mchache baada ya ajali hiyo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alitoa pole kwa Watanzania na wafanyabiashara ambapo pamoja na kueleza masikitiko yake aliwaagiza viongozi, vyombo vya ulinzi na usalama  pamoja na Jeshi la Uokozi kufanikisha zoezi la uokozi na tiba.

“Nimeuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, na Idara ya Menejimenti ya Maafa kufanya kila linalowezekana kufanikisha zoezi la uokoaji na tiba kwa majeruhi,” ameeleza Rais Samia aliye safarini kuelekea Brazil.

Aidha, Rais Samia amewataka Watanzania kuwaombea majeruhi kupata nafuu haraka hpamoja na kuwaombea subra ndugu jamaa, marafiki wanaotafuta riziki zao katika soko hilo la kimataifa.

Enable Notifications OK No thanks