Trump aweka historia mpya Marekani uchaguzi 2024

November 6, 2024 6:44 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link

Anakuwa Rais wa pili katika historia ya nchi hiyo kuongoza kwa vipindi viwili katika nyakati tofauti baada ya miaka 132.


Mgombea wa urais Marekani kwa tiketi ya Chama cha Republican, Donald Trump ameweka historia mpya kama rais aliyewahi kuitumikia nchi hiyo kwa awamu mbili katika nyakati tofauti tangu afanye hivyo Grover Cleveland miaka 132 iliyopita.

Katika matokeo ya uchaguzi wa taifa hilo kubwa dunia, Trump ameweka historia hiyo mara baada ya kushinda uchaguzi dhidi ya mshindani wake wa karibu na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Kamala Harris kutoka Chama cha Democratic.

Trump alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa rais mwaka 2016, akimshinda aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Hillary Clinton, nakuahidi kufanya Marekani kuwa bora tena “Make America Great Again.” 

Hata hivyo, alishindwa kutetea kiti hicho baada ya kupoteza uchaguzi wa urais dhidi ya Rais Biden mwaka 2020 wakati wa janga la kimataifa la Uviko 19 na kurejea tena katika kugombea nafasi hiyo ya urais mwaka huu.  

Uchaguzi mkuu wa Marekani mwaka huu ulifanyika jana Novemba 5 ukihusisha wagombea watano kiwemo mtoto wa Rais wa zamani wa Marekani Robert F. Kennedy Jr, Chase Oliver na Jill Stein kutoka Chama cha Kijani. 

Rais mteule Donald Trump akihutubia mara baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi wa Marekani. Viongozi mbalimbali wamempongeza kwa kushinda huku kukiwa na sintofahamu juu ya sera zake katika uhusiano wa kimataifa. Picha|USA Today.

Kurejea madarakani kunavyokumbusha historia

Kurejea kwa Trump katika Ikulu ya White House kunamfanya aingie kwenye historia ya pekee baada ya Cleveland ambaye alishika nafasi akiwa rais wa 22 na wa 24 wa Marekani. 

Alihudumu vipindi viwili visivyo mfululizo, jambo lililomfanya kuwa ndiye rais pekee katika historia ya Marekani kushika nafasi hiyo mara mbili kwa nyakati tofauti. Alikuwa rais kwa mara ya kwanza kutoka mwaka 1885 hadi 1889, kisha kuingia tena madarakani kutoka mwaka 1893 hadi 1897.

Ushindi wa Trump ni pigo jingine kwa Democratic ambacho kwa mara ya pili ndani ya miaka nane kinashindwa kushinda uchaguzi kikiwa kimesimamisha mgombea mwanamke.

Trump, aliyekuwa akipigiwa debe vilivyo na bilionea namba moja duniani, ameahidi kutekeleza sera za kukuza uchumi, kudhibiti wahamiaji na kutatua migogoro mikubwa duniani ikiwemo vita ya Urusi na Ukraine ndani ya muda mfupi. 

Hata hivyo, sera zake hazikuwa bayana zaidi juu ya uhusiano wake utakavyokuwa na mataifa ya Afrika ambayo yamekuwa yakivutana kuhusu nafuu za kibiashara na kutaka kuimarisha mahusiano ya kibiashara zaidi.

Viongozi mbalimbali duniani akiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wamempongeza kwa kuchaguliwa wakiahidi kufanya naye kazi katika kipindi cha uongozi wake wa miaka minne ijayo inayotarajiwa kuanza Januari 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks