Uchaguzi Marekani 2024: Trump ajitangaza mshindi, Harris akipambania majimbo muhimu
- Hadi sasa kura zinaendelea kuhesabiwa katika sehemu kubwa ya majimbo.
- Trump anazamiwa kushinda uchaguzi huo na kumwangusha mgombea wa Chama cha Democratic, Kamala Harris.
Mgombea wa urais wa Chama cha Republican nchini Marekani, Donald Trump amejitangaza mshindi wa uchaguzi huo baada ya Shirika la habari la Fox kutabiri kuwa atamshinda mshindani wake wa karibu wa Chama cha Democratic, Kamala Harris licha ya kura kuendelea kuhesabiwa.
Trump anatazamiwa kushinda uchaguzi huo baada ya kupata kura nyingi zaidi Harris, hatua inayompa fursa ya kuongoza taifa hilo kwa mara ya pili ndani ya miaka nane.
Hadi Saa 6:00 mchana kwa saa za Afrika Mashariki, kwa mujibu wa Shirika la habari la kimataifa la Reuters Trump alikuwa anaongoza kwa kura zaidi ya milioni 5.3 dhidi ya Harris ambaye alijitosa kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kujitoa kwenye mbio za urais.
Reuters imeripoti kuwa Trump alikuwa na milioni 69.66 sawa ana asilimia 51.1% ya kura zilizohesabiwa kutoka majimbo mbalimbali nchini humo huku Harris, ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais wa taifa hilo kubwa duniani, akiwa na kura milioni 64.39 sawa na (47.2%)
Kutokana na Trump kuongoza katika majimbo yenye kura nyingi za wajumbe (electorates votes), mwanasiasa huyo na mfanyabiashara mashuhuri duniani ana kura 266 ikiwa zimesalia kura 4 tu atangazwe mshindi.
Kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi wa Marekani, mshindi wa kiti cha urais anapaswa kupata kura za wajumbe 270 kati ya 538, ikiwa ni nusu ya kura zote jumlisha moja. Reuters wanabainisha kuwa Harris alikuwa ana kura za majimbo 219, akiwa nyuma ya Trump kwa kura 47 ambazo ni kutoka zaidi ya majimbo matano.
Hadi sasa, zoezi la uchaguzi nchini Marekani bado linaendelea kwa mchuano mkali katika baadhi ya majimbo muhimu, na matokeo bado yanatiririka.
Trump ajitangaza mshindi
Hata hivyo, Shirika la habari la Fox limesema linatazamia kuwa Trump atashinda uchaguzi huo jambo litakampa fursa ya kuongoza tena nchi hiyo baada ya kushindwa uchaguzi mwaka 2020.
Akiwa Palm Beach jimboni Florida, Trump amewaeleza wafuasi wake kuwa kwa sasa tayari ni mshindi kutokana na utabiri huo wa Fox licha ya kuwa kura kuendelea kuhesabiwa katika majimbo mengi ya nchi hiyo ya Kaskazini mwa bara la Amerika.
“Marekani imetupatia jukumu kubwa na lenye nguvu,” amesema Trump huku akishangiliwa na wafuasi wake mapema Jumatano hii.
Trump tayari ameshinda majimbo kadhaa muhimu kama Pennsylvania, Arizona, North Carolina na Georgia huku Harris akitarajiwa kushinda majimbo yenye mwelekeo wa chama cha Democratic kama New York na Hawaii.
Hata hivyo, majimbo mengine muhimu kama kama Pennsylvania, Michigan, na Wisconsin, ambayo yanaweza kubadili mwelekeo wa uchaguzi, bado hayajamaliza kuhesabu kura.
Majimbo hayo yanatarajiwa kuleta upinzani mkubwa kutokana na idadi kubwa ya kura za awali na za posta ambazo zinatakiwa kuhesabiwa ambazo kwa kawaida huwanufaisha wagombea wa chama cha Democratic.
Wachambuzi wameonya kuwa matokeo ya awali yanaweza kubadilika pindi kura zote zitakapohesabiwa, hasa kutokana na utaratibu wa kuchakata kura za posta unaochukua muda mrefu zaidi.
Hadi sasa Trump anaongoza kwa zaidi ya asilimia 52 katika jimbo la Michigan dhidi ya Harris ambaye ana zaidi ya asilimia 45.