Serikali kushusha gharama za matibabu ya figo
- Yatajwa kushuka kwenye hospitali mbili hadi sasa.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema ipo mbioni kupunguza gharama za matibabu ya wagonjwa wa figo nchi kutokana na baadhi ya wananchi kulalamikia gharama hizo kuwa juu.
Ugonjwa wa figo ni miongoni mwa magonjwa yasiyo ya kuambukizwa yanayotajwa kuathiri watu wengi nchini huku baadhi yao wakikosa huduma za muhimu ikiwemo kusafisha damu (dialysis) kutokana na gharama yake kuwa juu.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Godwin Mollel asilimia saba ya Watanzania wanaugua ugonjwa wa figo unaosababishwa na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukizwa.
Idadi hiyo ni sawa na kusema Watanzania milioni 4.3 kati ya Watanzania milioni 61.7 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 wanaugua ugonjwa wa figo.
Ili kukabiliana na gharama za kutibu ugonjwa huo nchini Dk Mollel amesema Serikali inatengeneza utaratibu mzuri wa kushusha gharama hizo huku baadhi ya hospitali zikiwa zimeanza kutoa huduma hizo kwa gharama nafuu.
“Tumeanza ndio maana ukienda kwenye baadhi ya hospitali zetu mkoa wa Dar es Salaam (hospitali mbili) sasa tumefanikiwa kuhakikisha tunashusha. Waziri ameunda tume inapitia kuja na makisio kuona tunapunguza wapi kwa sababu unaweza ukapunguza badala ya kupunguza ukaua mfumo wenyewe…
…na kuua mfumo utasababisha watu wakose kabisa huduma, ni bora wapate huduma kwa ghali lakini waendelee kuwa hai wakati tunaangalia mambo yanakwendaje, tunalichukua hilo tunaenda kulifanyia kazi na wiki ijayo tume italeta ripoti watupe njia ya kupunguza gharama,” amesema Dk Mollel.
Dk Mollel ameeleza mpango huo wa Serikali wakati akijibu maswali ya Wabunge waliotaka kufahamu mpango wa Serikali kupunguza gharama hizo leo Novemba 5, 2024 bungeni Dodoma.
Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Tabora Teska Mbogo (CCM) amefafanua kuwa gharama za kusafisha figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni Sh180,000 kila wakati mgonjwa atakapoenda kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, ili kudumisha afya ya figo zilizofeli mgonjwa anatakiwa kusafisha mara tatu kwa wiki hivyo kuhitajika kulipia Sh540,000 kiasi ambacho ni kikubwa sana kwa Mtanzania mwenye kipato cha kawaida.
Naye Jacqueline Kainja, Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Tabora (CCM) ameuliza kuhusu mpango wa Serikali kuwezesha hospitali zake kutoa huduma za kusafisha figo kwa gharama nafuu ili kuondoa adha wanayopata wagonjwa wakati wa matibabu.
Akifafanua kuhusu suala hilo Dk Mollel amesema ili kuwapunguzia wagonjwa mzigo wa matibabu njia moja wapo ni kuhakikisha bima ya afya inapatikana kwa watu wote.
“Lakini pia tunapambana kuhakikisha vifaa tiba, madawa na kila kitu tunakwenda kununua kiwandani moja kwa moja badala ya kununua kwa wauzaji wa kawaida ili kushusha gharama ya matibabu…
…lakini pia Serikali inautaratibu ndio maana kila hospitali ina maafisa ustawi wa jamii ambao wale wale watu wanaoshindwa kulipa kuna utaratibu wa kufuata ili waweze kutibiwa bila malipo,” amesema Dk Mollel.
Kwa mujibu wa Mollel kuongezeka kwa wagonjwa wa figo kunasababishwa na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukizwa hususan shinikizo la damu na kisukari, matumizi holela ya dawa hasa za maumivu, kutotumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi ipasavyo kwa waathirika.
Sababu nyingine ni kutozingatia mtindo wa maisha unaofaa kama matumizi makubwa ya vyakula vyenye chumvi na sukari nyingi, tabia bwete, unywaji wa pombe na matumizi ya tumbaku.