Wabunge waishauri Serikali njia za kuongeza pato la Mtanzania

November 4, 2024 7:33 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na Serikali kuongeza nguvu katika eneo la kilimo, uvuvi na ufugaji.

Dar es Salaam. Wabunge wa Tanzania wameishauri Serikali kuongeza uwekezaji katika kilimo, uvuvi na ufugaji kama njia ya kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja kwa kuwa sekta hizo zinaajiri watu wengi katika mnyororo wa uchumi.

Pato la Taifa la mtu mmoja mmoja (GDP Per Capita) ni kipimo kinachotumiwa kuonesha wastani wa pato kwa kila raia wa nchi kikiwa kimegawanywa kutoka pato jumla la Taifa ambapo kwa mwaka 2023 pato la Mtanzania lilikadiriwa kuwa Sh3 milioni kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi ya mwaka huo.

Pato hilo liliongezeka kwa Sh201,534 kutoka Sh 2.8 milioni iliyorekodiwa mwaka 2022.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wamebainisha kuwa kasi ya ukuaji wa pato la Taifa ni kubwa ukilinganisha na ile ya ukuaji wa pato la mtu mmoja mmoja wakipendekeza mbinu mbalimbali zinazoweza kuchochea ukuaji wa pato la mtu binafsi.

Mwaka 2023 pato la Taifa lilifikia Sh148.399 trilioni kutoka Sh141.247 ya mwaka 2022, sawa na ukuaji wa asilimia 5.1 ikilinganishwa na asimilia 4.7 mwaka 2022 ikikadiriwa kiwango hicho kuendelea kukua hadi asilimia 6.1 ifikapo mwaka 2025.

Mbunge wa Muleba Charles Mwijage alipokuwa akiwasilisha mapendekezo kwa Kamati ya Mipango leo Novemba 4, 2024 bungeni jijini Dodoma amesema ili kuongeza pato la mtu mmoja mmoja Serikali inapaswa kuongeza nguvu  katika uzalishaji na utoaji huduma hasa katika sekta za mifugo na uvuvi.

“Tanzania tunayo fursa ya mifugo…lakini ninazo taarifa kuwa Malaysia wanahitaji nyama kutoka Tanzania tani laki moja, leo tunauza nyama Dola milioni 57, tuwekeze zaidi kwenye sekta ya mifugo….

…Tanzania inatakiwa kuiga mfumo wa Zimbabwe mtengeneze ‘pastoral’ muwape ng’ombe wa kisasa wa maziwa watu wawe wanaingia na kuzalisha soko lipo,” amesema Mbunge wa Muleba Charles Mwijage.

Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Sekta ya Mifugo ya mwaka 2006, mifugo ina nafasi kubwa katika kujenga uchumi imara wa Taifa, kuongeza kipato kwa watanzania wanaotegemea mifugo na kutoa fursa ya ajira na kuhifadhi rasilimali za Taifa.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi inabainisha kuwa sekta ya mifugo kwa mwaka 2022 ilikua kwa asilimia 5 na kuchangia asilimia 6.7 kwenye pato la Taifa.

Kwa upande wake Mbunge wa Ludewa Joseph Kamonga amesema kuwa ili pato la mtu mmoja mmoja kukuwa ni vyema Serikali kuwekeza katika eneo la kilimo kwa kuwa ndio eneo ambalo Watanzania wengi hutegemea kujipatia ajira.

“Kilimo kimeajiri zaidi ya asilimia 65 hadi 70 ya Watanzania na kinatoa mchango mkubwa sana wa usalama wa chakula lakini vile vile kinachangia vizuri kwenye pato la Taifa sasa ili tuweze kuinua pato la mtu mmoja mmoja katika eneo hili la kilimo hasa tumsaidie mwananchi katika kuongezaa tija,” ameongeza Kamonga.

Kamonga amesema Serikali inapaswa kuelekeza fedha nyingi katika kuwezesha upatikanaji wa ruzuku ya pembejeo ili kuwapunguzia mzigo wa gharama za kilimo na kuchochea kilimo tija.

Aidha, Kamongo ameongeza, kwa kuwa nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikikumbwa na majanga ya ukame ni vyema Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kutafuta masoko ya nje ili kuuuza mazao ya chakula nje ya nchi.

Abdullah Mwinyi Mbunge wa Jimbo la Mahonda amebainisha kuwa maendeleo lazima yawe ya watu kwa sababu maendeleo ya vitu ni njia tu ya kupeleka maendeleo kwa watu akisisitiza Serikali kuwekeza katika utoaji wa huduma za elimu inayokidhi mahitaji ya soko la ajira.

“Lazima tuhakikishe vijana wetu wa Kitanzania wanazungumza lugha mbili angalau Kiswahili na Kiingereza,” amesema Mwinyi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks