SGR yafungua neema mpya kwa Watanzania

November 1, 2024 4:37 pm · Mlelwa Kiwale
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuongezeka kwa ajira na mapato kwa Serikali.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Maendeleo, Prof. Kitila Mkumbo ameelezea mafanikio ya uwekezaji wa mradi wa reli ya kisasa (SGR) ikiwemo kukuza uchumi wa Tanzania.

Prof Kitila aliyekuwa akizungumza leo Novemba 1, 2024 wakati akiwasilisha mapendekezo ya mpango wa Taifa wa maendeleo unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali 2025/2026 bungeni jijini Dodoma amesema tangu kuanza kutekelezwa kwa mradi huo tayari umeshatoa ajira 30,176 za moja kwa moja na ajira zaidi ya 150,000 zisizo za moja kwa moja.

“Mradi umetoa fursa kwa viwanda, wazabuni na wakandarasi ambapo hadi sasa jumla ya kampuni 2,460 zinashiriki katika mradi huu na kandarasi zenye thamani ya Sh 3.69 trilioni zimetolewa tangu mradi uanze,” amesema Waziri Mkumbo.

Ajira hizo zimetengeneza pato la Sh 358.74 bilioni kwa vijana wakitanzania jambo lililosaidia kukuza uchumi wao na pato la Taifa.

Prof Mkumbo ameeleza kuwa hadi kufikia Septemba 2024 jumla abiria 645,421 walisafirishwa na kuwezesha Serikali kukusanya kiasi cha Sh 15.695 huku Serikali ikitarajia kukusanya mapato zaidi kutokana na kuongezeka kwa biashara, utalii na uwekezaji mara dufu ya kile kinachokusanya sasa.

“Hadi kufikia Septemba 2024 jumla ya miradi 519 imesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji (TIC) katika ushoroba wa reli yenye kuvutia mtaji wa Dola za Marekani bilioni 4.59 na kutarajia kuzalisha ajira 115,566. Miradi hii ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji huku baadhi yake ikiwa imeshakamilika na kuanza uzalishaji”, amesema Waziri Mkumbo.

Mbali na kuongeza kipato na ajira mradi huo pia umechochea kuongezeka kwa mahitaji ya saruji, nondo na vifaa vingine vya ujenzi na kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi, kupunguza ajali na kuokoa maisha ya watu.

Kwa mujibu wa Prof. Mkumbo kupitia Shirika la Reli (TRC) inaendelea na ujenzi wa awamu nyingine wa Reli hiyo kwa vipande vya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza wenye urefu wa kilomita 1,219 na awamu ya pili kutoka Tabora hadi Kigoma wenye urefu wa kilomita 1,010.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks