Bunge la Tanzania kupokea uchambuzi wa taarifa ya CAG kuanzia kesho Oktoba 28, 2024.

October 28, 2024 5:41 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Miongoni mwa shughuli zitakazofanyika ni pamoja na kupokea taarifa za kamati za kudumu za bunge pamoja na maswali kwa Waziri Mkuu.

Arusha. Bunge la Tanzania linatarajiwa kuanza vikao vyake Oktoba 29 mwaka huu jijini Dodoma huku shughuli mbalimbali zikitarajiwa kufanyika ikiwemo kupokea na kuchambua taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2022/23.

Huenda uchambuzi huo wa taarifa ya CAG ikawa miongoni mwa mambo yanasubiriwa zaidi na wabunge pamoja na wananchi kutokana na kubainika kwa hasara na ubadhirifu wa mali za Serikali.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa ripoti hiyo kujadiliwa bungeni tangu iwasilishwe kwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan  Machi 28 mwaka huu na baadae Spika wa Bunge Tulia Ackson kutoa muda kwa kamati husika kuipitia na kuichambua.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano bungeni inabainisha kuwa mkutano huo wa 17 wa Bunge utamalizika Novemba 8 mwaka huu ambapo pia unatarajiwa kupokea na kujadili taarifa za kamati za tatu za kudumu za Bunge hilo.

“Katika Mkutano huu, Bunge litapokea uchambuzi wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) uliofanywa na Kamati ya Kudumu ya Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Hesabu zilizokaguliwa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.” imesema taarifa hiyo.

Bunge pia litapokea na kujadili taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Pamoja na shughuli hizo Bunge pia litakaa  kama Kamati ya Mipango kwa ajili ya kupokea, kujadili na kushauri kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa fedha 2025/2026. 

Aidha, wastani wa maswali 160 ya kawaida yanatarajiwa kuulizwa na kujibiwa na Serikali Bungeni huku mengine 16 yakitarajiwa kuulizwa kwa Waziri Mkuu pamoja na kuishauri Serikali kuhusu mwongozo wa uandaaji bajeti, vyanzo vya mapato, utekelezaji na vipaumbele vya mpango huo.

Enable Notifications OK No thanks