Serikali kuzindua vitambulisho vya kidijitali kwa machinga, wafanyabiashara wadogo Tanzania.

October 16, 2024 3:12 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Kuzinduliwa mkoani Arusha Oktoba 17, 2024.
  • Jumla ya machinga 45,283 wakiwemo wanaume 15,909 wameshasajiliwa mpaka sasa.

Arusha. Serikali ya Tanzania inatarajiwa kuzindua ugawaji wa vitambulisho vya kigitali kwa wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama wamachinga ili kurahisha zoezi la urasimishaji wa kundi hilo.

Zoezi hilo litalofanyika kesho Oktoba 17, 2024 jijini Arusha ni miongoni mwa ahadi alizotoa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Januari 25, 2022 wakati akizungumza na viongozi wa machinga jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Doroth Gwajima iliyotolewa leo Oktoba 16, 2024 inafafanua kuwa gharama ya utengenezaji wa kitambulisho hicho kitakachodumu kwa miaka mitatu ni Sh 20,000.

“Zoezi la utambuzi na usajili wa wafanyabiashara ndogo ndogo ni muhimu kwa kuwa litawezesha Serikali kupata takwimu sahihi ya kundi hili ambalo linajumuisha machinga, mama na baba lishe, wasusi, waendesha pikipiki za miguu miwili na miguu mitatu pamoja na makundi mengine ya wafanyabiashara ndogondogo,” imesema taarifa ya Gwajima.

Kwa mujibu wa Wizara hiyo mpaka sasa jumla ya machinga 45,283 wakiwemo wanaume 15,909 na wanawake 29,374 wameshasajiliwa katika mfumo utakaowawezesha kupata vitambulisho.

Aidha, Ugawaji wa vitambulisho hivyo utashirikisha vitengo na wizara nyingine ikiwemo Wizara ya Viwanda na Biashara, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Biashara pamoja na Maafisa TEHAMA waliopata mafunzo maalum.

Hata hivyo, Wizara hiyo imesema vitambulisho hivyo sio mbadala wa ada na tozo zinazotozwa na mamlaka za halmashauri hapa nchini katika maeneo biashara ndogo ndogo zinapofanyika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks