TMA yatahadharisha upepo mkali Pwani, Ziwa Nyasa

October 4, 2024 3:43 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani na Ziwa Nyasa yanatarajiwa kuwa na upepo mkali unaoweza kuhatarisha maisha ya wavuvi na watumiaji vyombo vya maji. 

Dar es Salaam. Baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na Ziwa Nyasa nchini yanatarajiwa kuwa na upepo mkali na mawimbi makubwa ndani ya siku 10 zijazo, jambo litakalohatarisha usalama wa wavuvi na watumiaji wa vyombo vya majini. 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema upepo huo unatarajiwa kufikia kasi ya zaidi ya kilomita 40 kwa saa, huku mawimbi yakitarajiwa kufikia urefu wa mita mbili.

Maeneo yanayotarajiwa kuathirika ni pamoja na mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba.

Kwa mujibu wa TMA mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria inayojumuisha Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara inatarajiwa kuwa na maeneo machache yatakayo kuwa na mvua na ngurumo.

Picha hii inaonesha baaadhi ya athari zinazoweza kusababishwa na upepo. Picha/ Disaster Kleenup Specialist.

Mvua nyepesi zinatarajiwa katika maeneo machache katika mikoa ya Nyanda za juu kaskazini mashariki inayojumuisha Arusha, Manyara na Kilimanjaro).

Katika Pwani ya kaskazini yaani  Tanga, Maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam Pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, TMA imesema inatarajia kuwa na mvua katika maeneo machache.

Katika jiji la Dar es Salaam tangu asubuhi ya Oktoba 4, Nukta Habari imeshuhudia mvua katika baadhi ya maeneo yakiwemo Magomeni, Mwananyamala, Kivule, Mbezi huku kukiwa na upepo mkali. 

TMA imesema inatarajia kuwa  mikoa ya Magharibi mwa nchi Kigoma, Katavi na Tabora itakuwa na mvua na ngurumo za radi katika maeneo machache.

Hata hivyo, wakazi wa mikoa ya Dodoma na Singida wanatarajiwa kuwa na hali ya hewa kavu. 

Nyanda za juu Kusini-magharibi inayohusisha mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa yenyewe ndani ya siku hizo 10 inatarajiwa kuwa mvua nyepesi katika maeneo machache.

Hali ni hivyo hivyo katika mikoa ya Mtwara na Lindi mvua zinatarajiwa katika maeneo machache.

TMA imeeleza katika taarifa yake ya utabiri wa hewa kuwa Kanda ya kusini (mkoa wa Ruvuma na Maeneo ya kusini mwa Morogoro) kutakuwa na mvua nyepesi katika maeneo machache.

Licha ya kuwa mvua ni furaha kwa baadhi ya watu ila pia kuna vilio vingi kutoka kwa baadhi ya watu kwa sababu ya madhara ambayo hutokana na mvua hizo. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks