Bashe: Tunafanya mabadiliko ya ununuzi, malipo vyama vya ushirika Tanzania

September 25, 2024 7:38 pm · Yuster Massawe
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema mfumo wa sasa wa malipo una ukiritimba.
  • Mfumo mpya kutumika malipo ya korosho, kahawa baada ya kufanyiwa majaribio.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inafanya mabadiliko ya mfumo wa ununuzi wa mazao na malipo ya wakulima kupitia vyama vya ushirika ili kukabiliana na ukiritimba na ubadhirifu wa baadhi ya viongozi wa vyama hivyo jambo litakalosaidia fedha kuwafikia wakulima kwa wakati na kuchochea maendeleo.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliyekuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye ziara ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, wilayani Mbinga mkoani Ruvuma amesema mfumo uliopo una mapungufu ikiwemo kuwa na mlolongo mrefu ambapo licha ya mnunuzi kulipa fedha kwa wakati baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika walichelewesha malipo kwa wakulima makusudi ili kutengeneza mianya ya ubadhirifu.

“Mfumo wa sasa hivi ni kwamba mnunuzi analipa kupeleka chama kikuu, chama kikuu kinapeleka chama cha msingi, chama cha msingi ndo kinalipa mkulima, tunapobadili mfumo wa uuzaji tunabadili na mfumo wa malipo…

…Mkulima akiuza kahawa yake mnadani, malipo yatatoka chama kikuu moja kwa moja kwenda kwenye akaunti ya mkulima hayatapitia kwenye chama cha msingi, tunaondoa huo ukiritimba ili kuondoa tatizo lililopo, amebainisha Bashe.

Kwa mujibu wa Bashe wanunuzi hutoa malipo yao baada ya saa 48 tangu mnada ulipofanyika ambapo fedha zikienda kwa vyama vya msingi hushikiliwa na baadhi ya viongozi jambo linalowavunja moyo wakulima ambao hutumia muda, nguvu na gharama zao kuandaa mazao na hutegemea fedha watakazozipata kujikwamua kiuchumi.

Bashe ameongeza kuwa wameshafanya majaribio ya mfumo huo mpya katika Mkoa wa Lindi ambapo wamepata matokeo chanya na hivyo Serikali inakusudia kuutumia katika ununuzi wa zao la korosho pamoja na kahawa.

Mikakati kupunguza gharama za kilimo yatajwa

Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayojihusisha na kilimo kwa kiasi kikubwa ambapo mazao ya chakula kama mahindi ndio huzalishwa kwa wingi na baadhi ya maeneo hulima mazao ya biashara kama kahawa ambapo baada ya kuvunwa huuzwa kupitia vyama vya ushirika.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Usalama wa Chakula iliyotolewa na Wizara ya Kilimo ya mwaka 2021/2022 mkoa wa Ruvuma ndio ulikuwa kinara katika uzalishaji wa mazao ya chakula ukizalisha jumla ya tani milioni 1.3.

Hata hivyo, wakulima wa mkoa huo wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ongezeko la gharama za kilimo kutokana na kupanda kwa bei za pembejeo na gharama za matayarisho ya shamba ambapo wameiomba Serikali kusaidia kuwapunguzia mzigo wa gharama ili wafanye kilimo kwa urahisi.

Kwa upande wake Waziri Bashe amesema ili kupunguza gharama za kilimo mkoani humo Serikali itajenga kituo cha zana za kilimo kitakachokuwa na matrekta pamoja na kuoongeza ujenzi wa maghala katika maeneo mbalimbali ili kupunguza gharama za usafirishaji wa nafaka.

“Bei ya kulimiwa kwa ekari, Rais Samia ametoa ruzuku, itakuwa Sh40,000 badala ya bei ya sasa mnayochajiwa ambayo ni Sh80,000 mpaka 120,000,” amesema Bashe.

Uzeni kwa NFRA

Aidha, Waziri Bashe ametoa wito kwa wakulima kuwa wavumulivu na kuuza mazao yao kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ambako watauza kwa bei ya juu kuliko kuwauzia walanguzi wanaounua kwa bei ya chini.

Kwa mujibu wa Bashe tangu kuanza kwa msimu mpya wa ununuzi NFRA mkoani humo imeshanunua tani 13,000 za mahindi na Sh10 bilioni imetolewa kwa wakulima.

“Nawaomba msiwapelekee mahindi madalali wanawadanganya kuwaambia kwamba utasafisha sana, unapoteza kilo 10 tu katika gunia la kilo 120, ambayo kwa bei yao umepoteza Tsh30,000. Yeye akiyanunua kwako kwa Tsh300 anakwenda kuyauza Tsh700 anapata zaidi ya Tsh200 ya faida, ni heri uvumilie wiki moja au mbili hiyo faida uichukue wewe kwasababu umeitafuta shambani kwa miezi sita,” amefafanua Bashe.

Hata hivyo, huenda katika baadhi ya maeneo wakulima hulazimika kuuza kwa walanguzi kutokana na umbali kati yao na vituo vya NFRA huku ubovu wa miundombinu ya barabara ukikwamisha zaidi juhudi hizo za Serikali ambapo Bashe amesema wanaifanyia kazi changamoto hiyo kwa kujenga maghala mapya na vituo vya NFRA katika maeneo mbalimbali.

Habari hii imeandikwa na Yuster Massawe na kuwekwa nyongeza na Davis Matambo

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV