‘Suluhu Sport Academy’ kukuza vipaji vya vijana Tanzania

August 22, 2024 6:38 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Kinatarajiwa kuwa kituo kikubwa cha kukuza vipaji vitakavyo shindana kimataifa.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kukamilika kwa akademia mpya ya michezo iliyopewa jina la Suluhu kutasaidia kukuza vipaji vya kimichezo vya vijana wa Tanzania.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika halfla ya kuweka jiwe la msingi akademia hiyo leo Agosti 22, 2024 Kizimkazi visiwani Zanzibar amesema kuwa akademia hiyo itasaidia kuendeleza vipaji vya wanamichezo nchini.

”Mungu ametubariki vipaji vingi vya wanamichezo tofauti, lakini kwasababu hatuwaendelezi wanaishia kwenya ngazi za chini tu hapa…juzi tumekwenda Olympic hatukuambulia kitu lakini wale walioambulia ni wale ambao wanawekwa wanafundishwa techniques (mbinu mbalimbali),” amesema Rais Samia.

Mwaka huu Tanzania ilipeleka wanamichezo saba kwenye mashindano ya Olympic yaliyofanyika Paris nchini Ufaransa ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 1980 wanamichezo wa wakati huo wapeperushe bendera ya Tanzania katika mashindano hayo.

Hata hivyo, wanamichezo hao walirudi mikono mitupu bila tuzo wala ushindi hatua iliyotafsiriwa na baadhi ya wadau wa michezo kuwa ni kukosa ubora na viwango vinavyohitajika katika mashindano hayo.

Kukamilika kwa akademia hiyo yenye viwanja vya mpira wa pete na kikapu, bwawa la kuogelea lenye kiwango cha Olympic kutawanoa wanamichezo wa Tanzania tayari kwa mashindano ya kimataifa.

Akademia hiyo pia itakua na jengo la utawala lenye ofisi 10, msikiti wa kuingiza watu 150, madarasa mawili ya kufundishia michezo, nyumba nane za wakufunzi, duka kubwa, sehemu ya mazoezi ya viungo (gym) na ukumbi wa mikutano utakaobeba watu zaidi ya watu 300.

Ramani inayoonesha mradi wa Suluhu ‘Sport Academy’.Picha| Ikulu Tanzania.

Rais Samia amewapongeza waanzilishi wa akademia hiyo inayotarajiwa kuwa kituo kikubwa cha mafunzo ya kimichezo ili kuwapa fursa vijana wenye vipaji kuongeza ubora wao wa ushindani kitaifa na kimataifa.

“Ulianza kama wazo dogo sana la Suluhu Sports Academy, hawakua na tamaa au fikra kama mradi huu utakuwa mkubwa kiasi hiki…lakini niwashukuru wadau wote wa maendeleo mliodaka wazo hili na mkasema mlikuze kwa kiwango hiki,” amesema Rais Samia.

Abdul Sekela, Mtendaji Mkuu wa benki ya CRDB amesema wao pamoja na wadau wenza wamechukua hatua ya kufadhili ujenzi wa akademia hiyo sambamba na viwanja vya kisasa vya michezo.

“Wadau wa maendeleo waliona ni bora wafanye jambo moja kubwa litakaloacha alama na kuendana na sera zako, ndio wakaja na wazo za kuanzisha Suluhu Sports Academy…wazo hili linakuja likiwa mtambuka kwa kujua kwamba kitakua ni kitovu na kituo kikubwa cha michezo mbalimbali,” amesema Abdul Sekela.

Mtendaji Mkuu wa CRDB amebainisha akademia hiyo inajengwa sambamba na uwanja mpira wa miguu wenye uwezo wa kubeba watazamaji 20,000 ukitarajiwa kumalizika Aprili 2025 na kutoa ajira 250 za kudumu na nyingi za muda mfupi pamoja na ujenzi wa mtandao wa kilomita 1.2 wa maji safi.

“Hii ‘phase’ awamu ya kwanza ni ya kujenga kiwanja kikubwa cha mpira chenye uwezo wa kuwa na watazamaji 20,000…kinakidhi vigezo vyote vya FIFA na kimataifa kwa hiyo sisi kama wadau tunajivunia sana wazo hili,” ameongeza Abdul.

Enable Notifications OK No thanks