Umeme wa gridi ya Taifa kukuza uchumi Katavi
- Mradi huo utagharimu Sh48 bilioni.
- Rais Samia aagiza Wizara ya Nishati, Tanesco kusimamia usambazaji wa umeme kwa haraka mradi ukikamilika.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema upatikanaji wa umeme wa gridi ya Taifa wa mkoani Katavi utachochea uwekezaji pamoja na kuwezesha wananchi kufanya shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato hivyo kukuza uchumi wa mkoa huo.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika kijiji cha Inyonga wakati akiendelea na ziara yake mkoani Katavi leo Julai 13, 2024 amesema kuwa mradi huo utakamilika mwezi Septemba mwaka huu na kuwawezesha wakazi wa mkoa huo kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Mwezi wa tisa mkoa huu, wilaya hii, itatumia umeme wa gridi ya Taifa tunakwenda kuachana na majenereta…Tuutumieni umeme kwa maslahi ya kiuchumi anayeweza kuweka saluni kukata nywele aweke, anayeweza kuchoma vyuma akatengeneza madirisha aweke, anayetaka kuchoma mageti afayanye,” amesema Rais Samia.
Kwa mujibu wa Rais Samia ujenzi wa mradi huo utagharimu Sh48 bilioni hadi kukamilika kwake na nyongeza ya Sh116 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa njia za umeme utakaopokea, kupoza na kupeleka umeme katika vituo vingine.
Rais Samia amewaambia wananchi wa Inyonga kuwa mkoa huo hutumia zaidi ya Sh2 bilioni kwa ajili ya kuendesha mitambo ya jenereta na kuwasha umeme kwa mwezi jambo linalochangia uharibifu wa mazingira pamoja na kuongeza gharama za kiuendeshaji kwa Serikali.
Soma zaidi:Digital connectivity is key to social, economic transformation in Tanzania
Huenda umeme wa gridi ya Taifa ukasaidia kukuza uchumi wa mkoa wa Katavi ambao kitabu cha takwimu za msingi za Tanzania kwa mwaka 2022 (Tanzania in Figures), kilichotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kinautaja kuwa miongoni mwa mikoa maskini Tanzania.
Takwimu za NBS zinabainisha kuwa Mwaka 2022 pato la mtu mmoja mmoja lilikuwa Sh1.9 milioni ambalo ni la chini kwa wastani wa pato la Taifa kwa asilimia 29.
Hata hivyo, Katavi ndio mkoa wenye baadhi ya huduma chache zaidi za kijamii nchini ikiwemo shule na vituo vya afya ambapo ina jumla ya shule 328 pamoja na vituo 134 vya kutolea huduma za afya, kiwango cha chini ikilinganishwa na baadhi ya mikoa mingine yenye idadi sawa ya watu.
Wananchi wa Inyonga mkoani Katavi wakishangilia baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwatembelea.PichaIkulu/X(Twitter).
Umeme kupaisha uwekezaji Katavi
Mbali na shughuli hizo, Rais Samia amesema kuwa umeme huo pia utaongeza shughuli za uwekezaji jambo linaloweza kuongeza ajira kwa vijana wa mkoa huo wenye kilomita za mraba 47,527.
“Umeme huu pia utakuza uwekezaji, pakiwa na umeme wa uhakikia ambao haukatiki wawekezaji watakuja na shughuli za uwekezaji zitaendelea vyema,”amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ameagiza Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kusimamia mradi huo ukamilike kwa wakati pamoja na kuratibu kwa haraka zoezi la kuunganisha na kusambaza umeme huo kwenye taasisi na makazi ya watu.
Latest