BOA Bank Tanzania yateua bosi mpya mwanamke
- Ni Esther Maruma ambaye anaongeza idadi ya viongozi wanawake katika sekta ya benki nchini.
- Atarajiwa kuongeza faida na wateja katika benki hiyo iliyokuwa na matawi 19 mwaka 2022.
Dar es Salaam. Bodi ya Wakurugenzi ya Bank of Africa (BOA) Tanzania imemteua Esther Maruma kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo na kumfanya kuwa miongoni mwa wanawake wachache wanaongoza taasisi za kifedha nchini.
Maruma anachukua nafasi ya Adam Mihayo aliyemaliza muda wa kuiongoza benki hiyo ya biashara hivi karibuni baada ya kuhudumu katika nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mei 6, 2024 na Mwenyekiti wa Bodi ya Bank of Africa Nehemia Mchechu uteuzi huo wa Maruma umeanza jana huku bodi hiyo ikiwa na imani kuwa uongozi wake wenye maono utainua hadhi ya benki hiyo sokoni na kuunda thamani ya kudumu kwa wadau wote.
Maruma ni miongoni mwa wanawake wachache wanaoongoza taasisi kubwa katika sekta ya fedha inayotawaliwa na idadi kubwa ya viongozi wanaume.
Uchambuzi wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) uliofanywa na Nukta Habari unabainisha kuwa kati ya benki 34 za kibiashara zilizosajiliwa Tanzania, ni benki tatu pekee zilizokuwa zinaongozwa na wanawake.
Mabosi hao wanawake wanaongoza benki za biashara ni Ruth Zaipuna, Mkurugenzi wa Benki ya NMB, Esther Mang’enya (Mkurugenzi wa Benki ya Azania) pamoja na Isabela Maganda ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity.
Kabla ya uteuzi huo, Maruma aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Masoko katika Benki ya Absa kwa miaka 15 ambapo bodi hiyo inaeleza kuwa alionesha mafanikio mashuhuri ikiwemo uanzishaji wa mikakati bunifu ya uuzaji uliopelekea ukuaji wa wateja na uboreshwaji wa bidhaa na huduma.
“Tunaamini uongozi wake utachukua jukumu muhimu katika kuharakisha ujumuishaji wa kifedha na kuongoza juhudi zetu kwa ujumla katika kuleta mabadiliko ya kidijitali,” amesema Mchechu katika taarifa hiyo.
Maruma, mwenye shahada ya kwanza ya sayansi katika Sayansi ya Mazingira na Usimamizi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, atakuwa na kibarua cha kuiongoza benki hiyo kuongeza wateja na faida zaidi kuliko mtangulizi wake.
Taarifa ya fedha za Bank of Africa Tanzania ya mwaka 2022 inaonesha benki hiyo ilirekodi faida ya Sh5.3 bilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 62 kutoka Sh3.3 bilioni iliyorekodiwa kwa mwaka wa fedha ulioishia Desemba 2021.