Bajeti Wizara ya Ulinzi yapaa kwa miaka minne mfululizo
- Yafikia Sh3.3 trilioni kutoka Sh2.9 trilioni ya mwaka 2023/24.
- Zaidi ya asilimia 90 yaelekezwa kwenye matumizi ya kawaida.
- Serikali yatakiwa kutoa fedha kwa wakati kwa wizara kutimiza mipango yake.
Dar es Salaam. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeliomba Bunge liidhinishe bajeti ya Sh3.3 trilioni kwa mwaka wa fedha 2024/25 huku asilimia 90 ya bajeti hiyo ikiwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Bajeti hiyo imeongezeka kutoka Sh2.9 trilioni ya mwaka 2023/24 ambayo ni ongezeko la Sh336.3 bilioni sawa na asilimia 11.2.
Ongezeko la bajeti katika wizara hiyo ni mara nne mfululizo tangu mwaka 2021/22 Serikali ilipoidhinisha Sh2.4 trilioni kwa ajili ya kufanikisha mipango ya wizara.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk Stergomena Tax, aliyekuwa akiwasilisha bajeti hiyo Bungeni jijini Dodoma leo Mei 20, 2024 amesema zaidi ya asilimia 90 ya fedha zilizoombwa zitaelekezwa katika matumizi ya kawaida.
“Sh3.008 trilioni sawa na asilimia 90.4 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh317.4 bilioni sawa na asilimia 9.5 ya bajeti ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” amesema Tax.
Endapo Bunge likipitisha bajeti hiyo, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa itaingia katika orodha ya wizara zenye bajeti inayozidi Sh1 trilioni katika mwaka ujao wa fedha.
Soma zaidi:Maeneo sita ya kipaumbele bajeti Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
Vipaumbele vya wizara kwa mwaka 2024/25
Kwa mwaka wa fedha 2024/25, wizara imejiwekea vipaumbele mbaimbali ikiwemo kuendelea kuliimarisha jeshi kwa zana na vifaa vya kisasa, mafunzo na mazoezi pamoja na rasilimali watu.
“Kuendelea kuweka mazingira mazuri ya utendaji wa kazi wa jeshi, kuimarisha miundombinu mbalimbali katika maeneo ya jeshi, kuimarisha mashirika na taasisi katika sekta ya ulinzi, kuendelea kushiriki katika ujenzi wa miradi ya kimkakati kwa maslahi mapana ya Taifa,” amesema Tax.
Wizara hiyo pia, itaendelea kuimarisha uwezo wa Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) liweze kuchukua vijana wengi zaidi, kufanya tathmini na kuandaa mpango mkakati kwa lengo la kuweza kuchukua vijana wote wanaostahili kupata mafunzo ya JKT.
Sambamba na hayo, itaimarisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya za Kikanda na nchi mbalimbali katika nyanja za kijeshi na kiulinzi na hivyo kuimarisha diplomasia ya ulinzi.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imeishauri Serikali kuendelea kuchukua hatua za kimkakati na madhubuti kuimarisha miundombinu ya ulinzi na kudhibiti mianya ya njia zisizo rasmi katika mipaka yetu, kufanya hivyo kutawezesha kudhibiti vitendo visivyo na afya kwa Taifa.
“Serikali itoe fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2023/24 kwa mashirika ya mizinga na nyumbu ili kutekeleza miradi iliyokusudiwa…
…Kufanya hivyo kutakuwa sehemu ya kuimarisha utendaji kazi,” amesema Minza Mjika Mjumbe wa kamati hiyo akimuwakilisha Mwenyekiti wake Vita Kawawa.
Latest